30 July 2012
Shindano la Maisha Plus 2012 kuja na sura mpya *Kipanya aomba sapoti kwa Watanzania kulifanikisha
Na Amina Athumani
KATI ya mashindano mbalimbali yanayoendeshwa hapa nchini shindano la Maisha Plus ambalo huendeshwa kwa kuoneshwa katika televisheni, limekuwa likiteka hisia mbalimbali za Watanzania hasa jinsi lilivyo na muonekano tofauti na mashindano mengine.
Shindano hili lilikuwa likifanyika kila mwaka kwa likishirikisha Watanzania kutoka mikoa mbalimbali ambao huingia katika kijiji cha mashindano cha Maisa Plus ambacho pia ni kama sehemu ya maisha ya kawaida ya kila siku anayoishi binadamu.
Baada ya kukosekana katika kipindi cha mwaka mmoja shindano hili limerudi na linatarajia kurushwa katika televisheni siku za hivi karibuni na kuteka hisia za mashabiki wa shindano hilo kama lilivyofanya katika miaka ya nyuma.
Mratibu shindano hilo, Masoud Ali 'Masoud Kipanya' anaelezea jinsi shindano hilo lilivyoboreshwa kwa mwaka huu wa 2012 na kusema kuwa hilo litaanza kurushwa tena mara baada ya kukamilika kwa usaili wake unaotarajiwa kuanza mapema mwezi Agosti.
Masoud anasema shindano hilo ambalo liliwahi kufanyika mara mbili, safari hii linakuja na nguvu mpya na burudani ya aina yake.
"Maisha Plus hatukulifanya mwaka jana, kuna marekebisho makubwa tumeyafanya ambayo yatalifanya hili liwe bora kuliko yaliyopita,"anasema Masoud maarufu kwa jina la Kipanya.
Ameongeza kuwa shindano hilo mwaka huu litaambatana na shindano dada la Mama Shujaa wa Chakula ambalo pia liliwahi kufanyika mwaka jana.
Katika muungano huo anesema washiriki wa Mama Shujaa wa Chakula wataingia katika kijiji cha Maisha Plus wiki mbili kabla ya kuanza rasmi kwa shindano hilo.
"Safari hii shindano tunaliunganisha na hili la Mashujaa wa Chakula linaloandaliwa na Oxfam ambao pia ni wafadhili wetu mwaka huu," anasema Kipanya.
Anasema Shindano hilo huwashindanisha wanawake wanaojihusisha na kilimo kidogo na limewahi kufanyika mwaka jana na Ester Jerome kuwa mshindi kutoka Dodoma na alijishindia zawadi ya trekta.
Anasema washiriki wa mashindano ya Shujaa wa Chakula wataingia kijijini na kukaa wiki mbili mpaka mshindi wao atakapopatikana na baada ya hapo watatoka na ndipo shindano rasmi la Maisha Plus 2012 litakapoanza rasmi.
Safari hii shindano hilo litawakusanya vijana kutoka mikoa 14 ya Tanzania Bara na Visiwani, baadhi ya mikoa itakayoshiriki ni pamoja na Morogoro, Dodoma, Tanga, Arusha, Moshi, Mbeya, Mtwara, Dar es Salaam, Zanzibar n.k.
Hii ni season ya tatu ya Maisha Plus, ya kwanza ilifanyika mwaka 2009 na mshindi alikuwa Abdulhalim Hafidh kutoka visiwani Zanzibar na ya pili ilifanyika 2010 ambapo alishinda Alex kutoka Mbeya.
Anasema Maisha Plus 2012 mbali na kuwa na washiriki wake 21 watakaoingia kijijini baada ya kufanyiwa usaili katika mikoa 13 ya Tanzania.
Anasema Usaili wa kwanza utafanyika Arusha Agosti 3 na Moshi Agosti 4 na katika Mkoa wa Tanga utafanyika Agosti 5 mwaka huu.
Mratibu huyo nasema vigezo vitakavyotumika kuwapata washiriki hao hautatofautiana na ule uliowapata katika mashindano mawili yaliyopita.
Vigezo hivyo ni umri kati ya miaka 21 na 26, mshiriki ni lazima awe mtanzania, awe na elimu siopungua ya SEkondari, awe anayejitambua na pia awe ni mchapakazi.
Kipanya anasema majaji wa Maisha Plus 2012 ni Kaka Bonda, Masoud Kipanya na Baby Madaha ambapo litakuwa likionyeshwa kila siku na TBC1 ambapo kipindi hicho kitaandaliwa na DMB Company LTD.
Kipanya anasema bila sapoti ya Watanzania hakuna kinachowezekana hivyo amewashukuru watanzania kwa kuwa watulivu katika kipindi chote cha mwaka jana ambacho shindano hilo halikufanyika huku akiwaomba watanzania kuendelea kusapoti shindano hilo ili liwe la kimataifa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Ningependa kujua umuhimu wa Mashindano haya ya Maisha Plus,kwa sababu mashindano mawili yaliyopita hayakuwa yakifundisha chochote watanzania.
ReplyDeleteMuandaaji wa mashindano haya,Bwana Masoud,alisema kuwa yalilenga kuwafundisha watanzania kuishi maisha ya uvumilivu katika maisha magumu.Lakini ukiangalia Maisha Plus ni ya kawaida sana ambayo watanzania huyaishi kila siku,vijijini na mijini.Kwa mfano,kuteka maji na kujitwisha kichwani,kukata kuni na kupika,ni shughuli za kawaida sana kwa jamii ya watanzania.Pengine mambo kama haya wangeonyeshwa wazungu na si watanzania.
Sijawahi kuona kipya katika mashindano haya.