30 July 2012
CWT yatoa notisi saa 48 za mgomo serikalini
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, jana imepokea notisi ya saa 48 inayohusu kusudio la walimu ambao ni wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kugoma kuanzia Julai 30 mwaka huu, saa moja na nusu asubuhi.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Peniel Lyimo, ilisema kabla notisi hiyo haijatolewa, Serikali imefanya jitihada za kujadiliana na viongozi wa CWT kuhusu jinsi ya kuboresha masilahi.
Alisema lengo ni kumaliza suala hilo kwa maelewano kwa kutumia vyombo na ngazi mbalimbali za kisheria ambapo shauri hilo liko Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ambapo jana saa tisa mchana pande zote zilifika Mahakamani.
“Mahakama iliamuru pande zote zikamilishe maelezo yao ifikapo Julai 31 mwaka huu, saa sita mchana ili kuiwezesha Mahakama iendelee kusikiliza shauri hilo na hatimaye kutoa uamuzi hivyo mgomo huo si halali kwa sababu shauri hili liko Mahakamani.
Alisema hatua ya CWT kutoa notisi ya kuanza kwa mgomo kabla ya kukamilika kwa shauri hili ni kukiuka taratibu halali za Kimahakama ambazo kila mmoja anawajibika kuziheshimu.
Aliongeza kuwa, Serikali inapenda kuwafahamisha walimu wote kuwa kujihusisha na mgomo huo ni kwenda kinyume cha Sheria, Kanuni na Taratibu za kazi hivyo wanapaswa kupima madhara ya mgomo usio halali na Serikali inawataka kuupuuza na kutoshirikiana na CWT bali walimu wote wanatakiwa kuendelea na kazi.
Wakati huo huo,
Mwandishi Jovither Kaijage, kutoka Ukerewe
anaripoti kuwa, asilimia 92.5 ya walimu katika Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza, wamepiga kura ya kuunga mkono mgomo ambao umeandaliwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT), ili kuishinikiza Serikali iboreshe masilahi yao.
Katibu wa CWT wilayani humo, Bw. John Kafimbi, aliyasema hayo wakati akizungumza na Majira juu ya hatua zilizofikiwa kati ya Serikali na chama hicho ili kutatua mgogoro wao.
Alisema baada ya pande hizo kushindwa kumaliza tofauti zao katika meza ya mazungumzo, wameamua kupiga kura ili kupata uhalali wa kwenda katika hatua ya mgomo.
Aliongeza kuwa, wanachama wa CWT wilayani humo ni 1,810 ambapo kura zilizopigwa 1,688 na kura za ndio 1,675 sawa na asilimia 92.5.
Bw. Kafimbi ambae ni mjumbe wa Baraza Kuu la CWT Taifa, alisema baada ya mchakato wa kupiga kura kukamilika, zitawasilishwa Makao Makuu ya chama hicho ili kumwezesha
Rais wao Bw. Gratian Mukoba kutoa tamko.
“Madai ya walimu ni nyongeza ya mshahara asilimia 100, posho za kufundishia masomo ya sayansi (55), sanaa (50) na ile ya kufanya kazi katika mazingira magumu asilimia 30,” alisema
Kutokana na hali hiyo, ameitauja jamii kutambua kuwa, walimu wamelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya Serikali kushindwa kutambua changamoto nyingi walizonazo pamoja na kukosa mahitaji ya msingi kama chakula na makazi.
Amewakumbusha walimu kutambua mgomo ambao utaitishwa utakua halali kwa sababu kabla ya kufikia hatua hiyo, CWT kimefuata taratibu zote kisheria ili kuondoa vikwazo ambavyo vinaweza kuzuia azma yao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment