17 July 2012
Bima ya kilimo iwanufaishe wakulima
Na Rehema Mohamed
KILIMO ni uti wa mgongo wa taifa kutokana na ukweli kuwa asilimia 80 ya wananchi hasa wa vijijini wanakitegemea kuendesha maisha yao.
Inadaiwa kuwa kabla ya uhuru kilimo kiliajiri zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wote na mazao ya katani, kahawa na pamba yaliongoza kulipatia Taifa fedha za kigeni.
Hali hiyo ilifanya kilimo kiendelezwe kwa kutumia mbinu mbalimbali za kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Kati ya miaka ya 1961 na 1980, zilibuniwa kaulimbiu na maazimio kama vile “Chakula ni Uhai”, “Siasa ni Kilimo”, “Kilimo cha Kufa na Kupona”, “Mvua za Kwanza za
Kupandia” ili kuhamasisha maendeleo ya kilimo, pamoja na kuhamasisha kilimo cha ujamaa.
Katika awamu ya tatu ya uongozi chini ya Rais Benjamin William Mkapa kilimo kilipata msukumo wa kipekee na kuwa chenye mafanikio.
Katika awamu hiyo utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Kilimo na Mifugo ya mwaka 1997 na uanzishwaji wa Mkakati wa
Kuendeleza Sekta ya Kilimo ulishuhudia kilimo kikikua kutoka chini ya asilimia 3 hadi asilimia 6.
Katika awamu ya nne ya uongozi chini ya Rais Dkt. Jakaya Kikwete, kilimo kimeendelea kupewa kipaumbele kikubwa, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) ambayo imekuwa chachu ya kuleta mapinduzi ya kijani hapa nchini bila ya kusahau sera ya Kilimo kwanza.
Jambo kubwa la kujivunia kutokana na kilimo ni kuwa kwa sasa asilimia 95 ya mahitaji ya Taifa ya chakula
kinazalishwa nchini.
Aidha, serikali imeweka mfumo wa kuhifadhi chakula kwa ajili ya matumizi wakati kuna upungufu wa uzalishaji.
Akiba ya Taifa ya Chakula imekuwa ikiongezeka kila mwaka ambapo inadaiwa uwezo wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula unatarajia kufikia tani 400,000 ifikapo mwaka 2015 kutoka uwezo wa kuhifadhi tani 150,000 mwaka 2009.
Mikakati mbalimbali inaendelea kutekelezwa hususan kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji, matumizi ya zana bora za kilimo na kuongeza upatikanaji wa pembejeo zinazohitajika katika kuongeza uzalishaji.
Mbali na hilo inadaiwa kuwa kilimo kinachukua takriban nusu ya pato zima la taifa na robo tatu ya bidhaa zote zinazouzwa nchi za nje.
Pamoja na kutoa chakula, kilimo vile vile kinatoa ajira kwa asilimia 80 ya Watanzania.
Sehemu kubwa ya kilimo nchini ni cha wakulima wadogo-wadogo ambao mashamba yao yana ukubwa wa kati ya hekta 0.9 na hekta 3.0 kila moja.
Karibu asilimia 70 ya ardhi ya ukulima wa mazao inalimwa kwa kutumia jembe la mkono, asilimia 20 kwa kutumia maksai na asilimia 10 kwa kutumia trekta.
Mbali na hilo kilimo cha Tanzania ni cha kutegemea mvua. Uzalishaji wa mazao ya chakula ndio unaoongoza katika uchumi wa Kilimo.
Hekta milioni 5.1 zinalimwa nchi nzima kila mwaka, na kati ya hizo asimilia 85 ni kwa ajili ya mazao ya chakula tu.
Inadaiwa kuwa wanawake ndiyo wafanyakazi wakubwa mashambani.
Matatizo makubwa yanayokabili Kilimo nchini Tanzania ni upungufu wa nguvu kazi na uzalishaji kutokana na uhaba wa nyenzo za kisasa za ukulima pamoja na kutegemea sana hali ya hewa ambayo haiaminiki.
Mazao na wanyama huathirika vibaya sana nyakati za ukame.
Kilimo cha umwagiliaji maji ndicho ambacho kinaweza kuinusuru Tanzania katika kuhakikisha uzalishaji usioterereka ili kujenga akiba nzuri ya chakula, pamoja na kuongeza kipato na kuboresha uzalishaji wa mazao kwa mkulima.
Hata hivyo ni jambo la kujiuliza,je ni wakulima wangapi nchini wana uwezo wa kuhimili kilimo hicho cha umwagiliaji?
Hivi karibuni, serikali ilitangaza kuanzisha bima kwa ajili ya Kilimo itakayowasaidia wakulima katika shughuli zao za kilimo.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Bima Nchini Bw.Israel Kamuzora akinukuliwa na vyombo vya habari alisema bima hiyo inayotarajiwa kuanzishwa hivi karibuni pia itawasaidia wakulima kupata mikopo ya kilimo.
Ni jambo la kupongezwa kwa serikali kuwakumbuka wakulima kwa kufikiria kuanzisha bima hiyo kwani kama itatekelezwa ipasavyo itakuwa msaada mkubwa kwa wakulima wetu nchini.
Hakika mikopo hiyo itasaidia wakulima kupata pembejeo nzuri za kilimo zitakazowezesha kuongeza uzalishaji na hatimaye nchi kuwa na uhakika wa chakula kwa msimu mzima wa mwaka.
Ni dhahiri kuwa bima kwa mazao ya kilimo ni muhimu kwa ajili ya uchumi kwani itasaidia kumuondolea mkulima hasara pindi ionapojitokeza hasa unapotokea ukame, hali mbaya ya hewa kama mvua nyingi na dhoruba zinayoweza kusababisha mazao kufa.
Serikali iwe makini na kuharakia uanzishwaji wa sera hii ili kuweza kuwakomboa wakulima kwa maendeleo ya Taifa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment