30 July 2012
Vitambulisho vya Taifa sasa vurugu tupu
Na Stella Aron
MCHAKATO wa ujazaji fomu za vitambulisho vya Taifa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, umegubikwa na utata mkubwa kutokana na fujo zinazotokea katika baadhi ya vituo.
Fojo hizo zinasababishwa na mrundikano wa watu ambapo hali hiyo ilijitokeza jana kwenye Kituo cha Mbezi Temboni.
Wakizungumza na Majira Dar es Salaam jana, wakazi wa Mbezi Temboni walidai kusikitishwa na idadi ndogo wa waandikishaji walioteuliwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Tiafa (NIDA) na kusababisha mrundikano wa watu vituoni.
Mkazi eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Bi. Hawa Hamisi, alisema idadi kubwa ya watu waliokuwa wakiandikishwa katika kituo hicho wanatoka maeneo ya suka, kwa msuguli, kibanda cha mkaa, kimara B na saranga.
“Leo (jana) ni siku tatu nashindwa kujiandikisha kutokana na wingi wa watu, nimelazimika kutoka nyumbani alfajiri ili kupanga foleni kama unavyoniaona lakini hadi sasa sijaandikishwa,” alisema.
Kutokana na vurugu hizo, baadhi ya viongozi wa NIDA walikwenda eneo hilo na kuongeza idadi ya waandikishaji.
Katika eneo la Mombasa, Ukonga pia kulikuwa na idadi kubwa ya watu hivyo kusababisha vurugu kutokana na idadi ndogo ya waandikishaji.
“Idadi kubwa ya watu tuliopo hapa ni wafanyakazi, leo tumepata nafasi ya kuja kujiandikisha lakini kama unavyoona hadi sasa hakuna dalili za kuandikishwa mbali ya kuja alfajiri.
“Tunaiomba NIDA iongeze waandishi ili mchakato huu uweze kufanyika kwa amani na utulivu kuliko ilivyo sasa,” alisema mkazi wa Mombasa, Bw. Ramadhabu Salum.
Hata hivyo, Mwandishi wetu pia alifika kwenye vituo vilivyopo maeneo ya Buguruni, Tandika, Kawe na Ubungo ambapo kulikuwa na msongamano mkubwa wa watu.
Kilio cha wananchi katika maeneo hayo ni idadi ndogo ya waandikishaji kama ilivyo katika vituo vingine hasa siku za mapumziko ambazo ni Jumamosi na Jumapili.
Kutokana na malalamiko hayo, baadhi ya wananchi wameiomba NIDA kuongeza muda ili kutoa nafasi kwa watu wengi zaidi kujiandikisha na kufanikisha mchakato huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment