29 June 2012

Wateja wote TANESCO kuunganishiwa umeme


Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limesema ifikapo kesho litakuwa limekamilisha kazi ya kuunganisha umeme kwa wateja wote walioomba kuunganishiwa nchi nzima.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Meneja Mahusiano kwa Umma wa shirika hilo, Bi. Badra Masoud, alisema hatua ni inatokana na vifaa vyote muhimu kuwasili nchini katika ofisi za kanda.


Alisema awali kazi hiyo ilikuwa ikikwamishwa na ukosefu wa vifaa lakini baada ya uongozi wa shirika hilo kukaa na kutafakari kwa kina kuhusu tatizo hilo, waliamua kununua vifaa hivyo.

“Hivi ninavyozungumza, nina hakika ifikapo Juni 30 mwaka huu, (kesho), wateja wote nchi nzima waliowasilisha maombi ya kuunganishiwa umeme, watakuwa wamepatiwa huduma hii,” alisema Bi. Masoud.

Aliongeza kuwa, tayari shirika hilo limesambaza vifaa muhimu zikiwamo nguzo na nyaya ili kuhakikisha wateja wate wanapata umeme.

“Kupitia mkakati huu, shirika pia limerejesha utaratibu wake wa kuunganisha umeme kwa mteja ndani ya siku 30 tangu awasilishe maombi kama ilivyokuwa awali.

“Shirika linahijitahidi kutekeleza maombi ya wateja ili kukidhi haja yao hivyo tunawasihi wateja wanapokuwa na matatizo, watoe taarifa mapema iwezekanavyo, pia tunatarajia kutoa namba zetu za simu ili pale wanapokuwa na matatizo watatuafute,” alisema.

Aliwahadharisha wananchi kuwa makini na matapeli maarufu kama  vishoka wanaojifanya watumishi wa shirika hilo na kuwaunganishia umeme jambo ambalo linaitia hasara shirika hilo.

Katika hatua nyingine, Bi. Masoud amewaonya watumishi wa shirika hilo ambao wanajihusisha na vitendo vya kuomba rushwa kwa wateja kwani vitendo hivyo vinaharibu sifa ya shirika.

“Yapo malalamiko mengi kutoka kwa wateja wanaodai kuombwa rushwa ili wapewe huduma, kuanzia mteja yeyote atakayeombwa rushwa atoe taarifa Makao Makuu ya TANESCO,” alisema.

No comments:

Post a Comment