07 June 2012

Walimu Wilaya ya Kahama uwe mfano wa kuigwa



WALIMU wa Shule za Sekondari wilayani  Kahama mkoani Shinyanga ,wameanzisha kampeni ya kupiga vita tatizo la mimba kwa wanafunzi mashuleni.

Mpango huo ambao wanauitwa 'Rosebug'  kwa maana 'ua waridi changa lazima litunzwe na kulindwa', lengo lake ni kuwaokoa watoto na tatizo la kupata ujauzito wakiwa shuleni.


Kampeni hiyo ilizinduliwa juzi katika Sekondari ya Nyihogo mjini Kahama na kuzihusisha shule 15 za Tarafa ya Kahama Mjini, ambapo kulitolewa elimu ya kuwataka watoto kuachana na vitendo vya zinaa vinavyosababisha mimba shuleni.

Tunaunga mkono mpango huo kwani tunatambua athari za mimba mashuleni. Ujauzito kwa wanafunzi kwa kiasi kikubwa unaathiri mipango ya wazazi wanafunzi kwa ujumla, ndiyo maana Serikali imekuwa mstari wa mbele kupambana na mafataki.

Tatizo hilo limekuwa likisababisha kila mwaka maelfu ya wanafunzi wa kike kuacha masomo kutokana na kupata ujauzito.

Tatizo hilo si tu linawasikitisha wazazi waliotumia fedha zao nyingi  kuwasomesha watoto wao, bali pia wanakuwa wameongezewa mzigo wa malezi ya mtoto.

Hali hii  huwakatisha tamaa wazazi na ndio sababu baadhi yao  wanahofu kuwaendeleza watoto wao wa kike kielimu.

Zipo sababu nyingi ambazo zimekuwa zikiwafanya mabinti wengi wajikute wakipata ujauzito na miongoni mwake ni kutokana na kutojua njia dhabiti za kujikinga na ujauzito na baadhi ya wazazi wanakaa mbali na watoto wao, hivyo kutopata fursa ya kuwapa elimu ya kujikinga na mimba za utotoni.

Wengine wanadhani jukumu hilo ni la walimu. Hali hiyo ndiyo inachangia kuongezeka kwa mimba kwa wanafunzi kutokana na watoto wetu kukosa malezi ya pamoja. Tunatambua kuwa zipo njia za kila aina ambazo zinaweza kumaliza tatizo hili iwapo kila mmoja ataelewa kuwa tatizo hilo ni kubwa.

Kinachotakiwa ni wazazi na walezi kwa pamoja ndani ya jamii ni kuzungumza kauli ya kutokomeza ujauzito kwa wanafunzi wa kike. Hii inawezekana iwapo kila mmoja wetu anatahakikisha mtoto wa jirani yake analindwa.

Hata hivyo tuna imani kama jitihada za pamoja zitaunganishwa kufanya kampeni kama hiyo, tatizo hili  litaweza kupungua kwa kiasi kikubwa kama  siyo kutokomezwa kabisa.

Tunachukua fursa kuwaomba walimu  na wazazi katika wilaya nyingine nchini nao kupanga mkakati kama huo ili kukabiliana na janga hilo.


1 comment:

  1. SHULE ZOTE ZA KATA ZIWE NA HOSTEL KWA WATOTO WA KIKE ,WAALIMU WA VODA FASTA KWA NGAZI WA STASHAHADA WARUHUSIWE KUKAMILISHA MAFUNZO ILI WAWE NA MAADILI YALIYOKUBALIKA

    ReplyDelete