14 June 2012

Wakulima Shinyanga watakiwa kuuza pamba bora isiyochafuka


Na Suleiman Abeid, Shinyanga

WAKULIMA wa zao la pamba mkoani Shinyanga, wametakiwa kuuza pamba yenye ubora na kushirikisha wadau ili kudhibiti uchafu wa zao hilo unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya wakulima wanapokwenda kuiuza sokoni.


Wito huo umetolewa juzi na Meneja Uendeshaji wa Kiwanda cha Kuchambua na Kusindika zao hilo cha Afrisian Ltd, kilichopo mjini hapa, Bw. Hrishikesh Katre, katika hafla fupi ya kukabidhi zawadi kwa vituo vya ununuzi wa pamba vilivyofanya vizuri msimu uliopita.

Alisema kama wakulima na wadau wengine watadhibiti uchafu wa zao hilo unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya wakulima ili kuongeza uzito wa pamba wanapokwenda kuiuza sokoni thamani yake katika soko la dunia itaongezeka.

Aliongeza kuwa, baadhi ya wakulima wamekuwa na tabia ya kuweka michanga, maji au magadi katika pamba kabla hawajaenda kuiuza sokoni kitu ambacho mbali ya kushusha ubora wake, pia husababisha hasara kwa kampuni zinazoinunua na serikalini.

“Suala la kurejesha ubora wa pamba yetu lipo mikononi mwetu sisi wenyewe wakulima na wadau wa zao hili, tukidhibiti uchafuzi huu pamba ambayo itanunuliwa itakuwa safi na ubora wake utakuwa mzuri hivyo bei katika soko itapanda na wakulima kufaidika,” alisema Bw. Katre.

Alisema kampuni hiyo imeanzisha utaratibu wa kuvizawadia vituo vyake vya ununuzi ambavyo hununua pamba safi isiyo na uchafu pamoja na kuwapa motisha watu wanaosimamia vituo hivyo kuhakikisha wananunua pamba safi.

Katika hafla iliyofanyika juzi kampuni hiyo ilitoa zawadi mbalimbali kwa wahasibu wa vituo hivyo ikiwemo pikipiki mbili aina ya Toyo, baiskeli mbili aina ya Phoenix, majembe manne ya kukokotwa na ng’ombe na simu tano za mkononi aina ya Nokia vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 4.8.

Bw. Katre alivitaja vigezo vinavyomfanya Mhasibu aweze kushinda na kupewa zawadi kuwa ni pamoja na kufikia lengo la makisio ya ununuzi wa pamba katika kituo chake.

Vigezo vingine ni uaminifu anapokabidhi pamba yake kiwandani na kuhakikisha hanunui pamba iliyochanganywa na mchanga, kokoto au kuwekwa maji ya magadi.

Aliongeza kuwa, kampuni hiyo inanunua pamba katika mikoa ya Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mwanza na tayari imeingia mikataba na vikundi 256 vya wakulima ambavyo vitapatiwa pembejeo za kilimo  katika msimu wa mwaka 2012/2013.

No comments:

Post a Comment