26 June 2012
Wagonjwa waanza kutolewa hospitali
Stella Aron na Rehema Maigala
MGOMO baridi wa madaktari ulioanza Juni 23 mwaka huu, katika baadhi ya hospitali nchini, umeanza kushika kasi na kusababisha baadhi ya ndugu kuhamisha wagonjwa wao baada ya kukosa huduma za matibabu.
Wakizungumza na Majira Dar es Salaam jana, baadhi ya ndugu wenye wagonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), walisema kama mgomo huo utaendelea, utasababisha wananchi wengi kupoteza maisha kwa kukosa huduma.
“Tunaomba huduma kwa madaktari lakini wanatuangalia tu na kutueleza kuwa, kwanini hatusikilizi vyombo vya habari juu ya kuwepo mgomo hivyo hawawezi kutoa huduma hadi Serikali itakaposikiliza madai yao,” alisema mkazi wa Mbezi, Bi. Harieth Timotheo, ambaye alitakiwa kufanyiwa upasuaji wa tumbo jana.
Naye Bi. Zuhura Abdallah, mkazi wa Kimara alidai kusikitishwa na kitendo cha madaktari kuchukua uamuzi wa kugoma na kusababisha wagonjwa wengi kukata tamaa kutokana na mateso wanayopata.
“Mgonjwa wangu alifanyiwa upasuaji wiki iliyopita hapa Muhimbili na amelazwa wodi ya MOI lakini ameshindwa kuongezewa dawa kwa sababu hakuna daktari wa kumuhudumia,” alisema.
Katika Hospitali ya Amana, waandishi wetu walishuhudia eneo la kuegesha magari ya madaktari kuwa jeupe ambapo baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo, walisema madaktari hawajafika kazini.
“Kama mnavyoona, eneo la kuegesha magari yao jeupe kabisa, mara nyingi siku za Jumatatu (jana), kuna magari mengi na mrundikano wa wagonjwa, hii inaoesha dalili ya mgomo huu kushika kasi kama mlivyosikia katika vyombo vya habari,” alisema mtumishi mmoja ambaye hakutaka jina lake halikupatikana mara moja.
Hali ya huduma katika Hospitali ya Temeke ilikuwa tofauti na hospitali nyingine ambapo madaktari walikuwa wakiendelea kutoa huduma. Waandishi wetu walishuhudia wagonjwa wakiingia na kutoka katika vyumba vya madaktari ambapo mrundikano wa wagonjwa ulikuwa mkubwa.
Katika Hospitali ya Mwananyamala, dalili za kuwepo mgomo baridi zilikuwa zikionekana kutokana na malalamiko ya wagonjwa.
“Kama yangu ni mgonjwa na leo asubuhi alitakiwa kuonana na daktari lakini hadi sasa (saa saba mchana), nimewasiliana naye amedai bado hajaonana naye,” alisema Bw. Yusuf Hashimu.
Madaktari wanaofanyakazi kwa vitendo, nao wameanza mgomo hadi Serikali itakaposikiliza madai ya madaktari. “Sisi hatufanyi kazi labda zile za dharura hadi Serikali itakaposikiliza madai ya wenzetu,” alisema daktari mmoja wa Hospitali ya Muhimbili.
Waandishi wetu walishuhudia katika hospitali zote wagonjwa wakipokelewa kama kawaida isipokuwa baadhi ya huduma.
Majira lilipomtafuta Msemaji wa Hospitali ya Muhimbili, hakuweza kupatikana ili kuzungumzia sakata hilo haata alipopigiwa simu ya mkononi, ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
Wakati huo huo, Mwandishi Esther Macha, anaripoti kutoka Mbeya kuwa, licha ya Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa jijini humo, Dkt. Eliuter Samky, kuwataka madaktari wote kurejea kazini, hali ya matibabu bado tete.
Katika kitengo cha wazazi, baadhi ya wagonjwa waliozungumza na Majira, walidai kukosa huduma kutokana na mgomo huo.
Katika Hospitali Meya mkoani hapa, kuna tangazo linalowataka madaktari kurejea kazini mara moja ambapo kutokuwepo katika eneo la kazi ni kinyume na taratibu za kazi zilizowekwa na Serikali.
Wakizungumza na Majira, wanawake wajawazito walidai kukosa huduma bila kupata matibabu yoyote kutokana na mgomo huo hivyo wagonjwa wanalazimika kurudishwa nyumbani.
“Hakuna huduma yoyote kama unavyoona, tumekaa hapa tangu saa moja asubuhi lakini hakuna daktari hata mmoja,”alisema Bi. Mariam Christopher.
Mmoja wa wauguzi wa hospitali hiyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema hali inatisha kwani madaktari wote licha ya kutakiwa warudi kazini, bado wamekaidi.
Kutokana na hali hiyo, wagonjwa wengi wanalazimika kwenda Hospitali ya Mkoa ambako ndiko kwenye huduma hasa kwa wanawake wajawazito.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

NIWAULIZE SERIKALI IWAPO WANAJESHI WAKIGOMA HATUA GANI INACHUKULIWA JE DAWA NI KUMLAZIMISHA AENDELEE NA MAPAMBANO?? MWALIMU ANAWEZA KUGOMA WAKAFUNDISHA UONGO ATHARI NI ZA BAADAYE MGANGA AKIGOMA NI HATARI SANA KUMLAZIMISHA JE AKITOA DAWA TOFAUTI KWA MAGONJWA TOFAUTI WATANZANIA HATUTAANGAMIA ?? WATANZANIA TUNAOMBA SANA TUSIFANYIWE KITEGA JARIBIO [EXPERIMENT CONTROL] TUNAWEZA KUZALISHA UGONJWA HATARI KULIKO UKIMWI
ReplyDelete