26 June 2012

Hukumu ya Malanda wizi wa bil. 2.2/- kutolewa leo



Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, leo inatarajiwa kutoa hukumu ya kesi ya wizi wa sh. bilioni 2.2 za Akaunti ya Madfeni ya Nje (EPA), iliyopo katika Benku Kuu (BoT), inayomkabili kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Rajabu Maranda na binamu yake Bw. Farijala Hussein.

Washtakiwa hao tayari wanatumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa sh. bilioni 1.8 za EPA, katika mahakama hiyo na kuhukumiwa Mei 23,2010.


Awali hukumu hiyo ilipangwa kutolewa Mei 17 mwaka huu na kiongozi wa jopo la Mahakimu watatu wanaoisikiliza wakiongozwa na Jaji Fatma Masengi lakini ilishindikana baada ya Mahakimu wawili katika jopo hilo kuugua.

Washtakiwa hao wanatetewa na wakili, Bw. Majula Magafu, ambapo katika utetezi wake Bw. Maranda akiongozwa na wakili wake aliiomba Mahakama itupilie mbali ushahidi wote ambao umetolewa na upande wa mashtaka kwa sababu yeye hakuwahi kuiba wala kughushi nyaraka mbalimbali. 



Bw. Maranda alidai kuwa, si kweli kwamba aliwasiliana na BoT kwa njia ya Septemba 8,2005 bali alisaini nyaraka baada ya kushawishiwa na Bw. Biswalo Mganga Kachele na Bw. Mkonyi baada ya kuambiwa malipo yaliyofanyika ni halali.

Alisema yeye ni mmoja kati ya watu waliosaini hundi za kuwalipa watu lakini hakuwahi kwenda BoT, bali waliokuwa wakienda huko ni Bw. Paulo Thobias na Bw. Fundi Kitunga.

Aliongeza kuwa, wakati fedha hizo zinachukuliwa kampuni ilikuwa chini yake na Bw. Hussein lakini fedha hazikuwa za kwao.

Kwa upande wake, Bw. Hussein aliiomba mahakama itupilie mbali ushahidi uliotolewa na mashahidi upande wa mashtaka kwa sababu hakuna fedha iliyoibwa na yeye hakuwahi kuiba wala kughushi.


Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuiba fedha hizo baada ya kudanganya kuwa kampuni yao ya Money Planners & Consultant, ilipewa deni na Kampuni ya B. Grancel ya nchini Ujerumani.

No comments:

Post a Comment