26 June 2012
Wachezaji gofu watakiwa kuchangamkia Kenya Open
Na Mwali Ibrahim
CHAMA cha Gofu Wanawake Tanzania (TLGU) kimewataka wachezaji wa mchezo huo kujitokeza kushiriki katika mashindano ya Kenya Open yanayotarajiwa kufanyika Juni 30 hadi Julai Mosi mwaka huu nchini Kenya.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa chama hicho Mbonile Barton alisema hiyo ni nafasi nzuri kwa wachezaji kuweza kujiongezea kiwango na kujitathimini hatua waliyofikia kimchezo.
"Wachezaji wajitokeze kwa wingi kushiriki katika mashindano hayo ambayo hayana kiwango cha wachezaji, kwani yatawasaidia katika kujiwekea rekodi ya kushiriki katika michezo mingi na hata kujiongezea uwezo katika kushiriki mashindano ya Kimataifa," alisema.
Alisema, Mashindano kama hayo pia yatawasidia katika kupata nafasi za kualikwa katika mashindano mbalimbali ikiwa ni pamoja hata ya kuwa miongoni mwa wachezaji wa timu ya Taifa.
"Wasiogope kutumia gharama zao katika mashindano makubwa kama hayo ambapo pia yatawasaidia katika kukutana na wachezaji wengine na kuweza kubadilishana nao mawazo na kujifunza mbinu nyingine mbalimbali za mchezo huo," alisema.
Mbonile alisema pia itawasaidia kuingia katika mchakato wa kuwa mchezaji bora kwani sifa moja wapo ya kuingia katika mashindano hayo ni kushiriki katika mashindano mengi kwa mwaka husika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment