13 June 2012
Usajili wa Yondani wamgusa Tenga
Na Zahoro Mlanzi
KATIKA kile kinachoonekana kuguswa na sakata la usajili la beki wa timu ya Taifa (Taifa Stars) na Simba, Kelvin Yondani, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, amesema suala hilo lina mwisho wake kwani chombo husika kitalifanyia kazi pale muda utakapofika.
Beki huyo hivi sasa amekuwa gumza si katika vyombo vya habari hata katika baadhi ya mitaa nchini kutokana na namna ambavyo inadaiwa kusajiliwa na Yanga akitoroshwa kambini usiku.
Kutokana na tukio hilo, uongozi wa Klabu ya Simba, ilitishia kuishtaki Yanga kwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kutokana na kushindwa kufuata taratibu husika.
Akijibu swali kuhusu sakata hilo Dar es Salaam jana, Tenga alisema Yondani hajatoroshwa kama inavyodaiwa ila anachofahamu ni kwamba beki huyo ni mtu mkubwa ambaye anaweza kuamua lolote, hivyo hakutoroka ila aliondoka kambini.
"Mimi ninadhani tuna mambo mengi ya kufanya kuliko kuanza kuzungumzia hili la Yondani, hiki ni kipindi cha usajili la lolote linaweza kuzungumzwa, si kitu cha ajabu mchezaji kutoka timu moja kwenda nyingine," alisema Tenga na kuongeza;
"Ila hapa tatizo ni kwamba ametokaje kambini, je alipewa ruhusa na viongozi wake au alijiondokea tu na hilo tumewaachia viongozi wake walishughulikie na litakapokamilika watatupa majibu ya hatua gani wamechukua."
Alisema usajili una taratibu zake na muda wake hivyo kama mchezaji akiwa na mkataba atacheza lakini asipokuwa nao hawezi kucheza na kwamba ndio maana suala hilo la usajili lipo mikononi mwa klabu zenyewe.
Alisema ana imani muda ukifika hakuna shaka chombo kinachohusika kitalifanyia kazi na mwisho wa siku itajulikana atachezea klabu ipi lakini yanayoendelea hivi sasa ni 'unazi' wa mashabiki wa klabu hizo.
Aliongeza kutokana na tukio hilo, hivi sasa wameingia mikataba maalum na wachezaji wao ambao utakuwa ukiwaelekeza taratibu za kambi, hivyo mchezaji akienda kinyume na taratibu hizo hatua za kuchukuliwa zitakuwa wazi.
Mbali na hilo, Tenga aliipongeza timu ya Taifa (Taifa Stars) kwa ushindi walioupata wa mabao 2-1 dhidi ya Gambia na kwamba ameomba kikosi hicho kilicho na vijana wengi kilelewe ili baadaye ilete matunda kwa taifa.
Alisema amekoshwa na kiwango kilichooneshwa kwani hakuaimini kama wangeshinda katika mchezo huo lakini kutokana na kujituma katika dakika zote 90 ndivyo zilizosababisha kupata matokeo mazuri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
TAARIFA HII KIDOGO INAONYESHA NI YA TENGA ZINGINE ZAONEKANA ZA KIZUSHI ZAIDI ZIKIZINGATIA BIASHARA ZAIDI KULIKO UKWELI
ReplyDelete