26 June 2012

TBL yajivunia tuzo ya dhahabu


Na Mwandishi Wetu

TUZO ya dhahabu ya kimataifa iliyochukuliwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Ndovu Special Multi, imewasili nchini juzi huku kampuni hiyo ikijivunia mafanikio ya bia hiyo kwa kutwaa mara mbili mfululizo.

Akizungumza Dar es Salaam jana mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Meneja wa bia hiyo, Bi. Pamela Kikuli alisema kampuni imefurahishwa na ushindi huo wa mara ya pili na kwamba tuzo hiyo imeiletea sifa nchi na kuitangaza kimataifa.

Alisema tuzo hiyo inajulikana kama “Grand Gold Award” ambayo hushindanisha bidhaa kutoka mataifa mbalimbali ambapo  Aprili, mwaka huu bia hiyo ilitangazwa rasmi kuwa mshindi wa tuzo hiyo.

Bi. Pamela akifafanua zaidi kuhusu tuzo hiyo alisema ni tuzo ya juu katika tuzo za bidhaa za kimataifa zinazotolewa na Taasisi ya Kimataifa inayoangalia ubora wa bidhaa ya ‘Monde Selection International Quality Institute’ iliyopo Athens, Ugiriki.

Naye Mpishi Mkuu wa bia wa TBL, Bw. Gaudence Mkolwa, alisema wamefurahishwa na ushindi huo na wana haki ya kusheherekea kwa kuitembeza tuzo hiyo maeneo mbalimbali ili Watanzania wajivunie bia hiyo.

“Tunayo kila sababu ya kusherehekea ushindi huu na tutapita kuitembeza tuzo hii kwa wateja wetu ili tusherehekee pamoja mafanikio ya kazi nzuri iliyoungwa mkono na wateja wetu kwa kunywa bia hii,” alisema Mkolwa.

Akikabidhi tuzo hiyo, Meneja wa wateja wa Kampuni ya Kimataifa ya Kusafirisha Mizigo (DHL Express), Bw. Busegi Kulwa, alisema kampuni yao inajisikia faraja kutokana na mafanikio waliyoyapata TBL kimataifa.

Alisema kampuni yao ina mtandao wa vituo 35 ikiwemo Tanzania, hivyo watahakikisha kufikisha huduma zao kwa wakati kwenye vituo vyote ili kwenda sawa na wateja wao.

No comments:

Post a Comment