26 June 2012
Sakata la umri wa Lulu,serikali yakimbilia mahakama ya Rufani
Na Rehema Mohamed
UPANDE wa mashitaka katika suala la utata la umri wa Msanii maarufu wa filamu Elizabeth Michael 'Lulu' umewasilisha mahakama ya Rufani maombi ya kuitaka mahakama hiyo ipitie upya uamuzi wa Mahakama Kuu wa kukubali kusikiliza utata wa suala hilo.
Wakili wa serikali Elizabeth Kaganda alieleza hayo jana mahakamani hapo mbele ya Jaji Dkt.Fauz Twaib wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutolewa uamuzi.
Kaganda aliiambia mahakama hiyo kuwa tayari wameshawasilisha maombi hayo mahakamani hapo na kupewa namba 6/2012 hivyo aliiomba mahakama hiyo isitoe uamuzi hadi hapo mahakama ya rufani itakapopitia upya maamuzi hayo.
Alidai katika maombi yao waliyowasilisha ,wanaomba makahama ya rufani iwape muongozo kuhusu uamuzi uliotolewa na Jaji huyo
Hata hivyo mmoja wa mawakili wanaomtetea Lulu Kanedy Fungamtama alipinga maombi ya upande wa mashitaka kwa kuwa maombi hayo yamewasilishwa hatua za mwisho.
Wakati huohuo mahakama hiyo pia imetoa amri ya kuitaka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusitisha kutaja shauri hilo hadi Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi wa suala la umri wa msanii huyo.
Juni 11, mwaka huu mahakama hiyo kupitia Jaji Dkt.Twaib ilitoa uamuzi wa kukubali kushughulikia sakata la umri wa msanii huyo.
Jaji Twaib alisema, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilikosea kukataa kuchunguza umri wa mshitakiwa huyo mbele ya Hakimu Augustina Mmbando.
Lulu anakabiliwa na kesi ya Mauaji ya Msanii mwenzake Steven Kanumba yaliyotokea Aprili 7, mwaka huu katika eneo la Sinza Vatican, Dar es Salaam.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 9, mwaka huu itakapoletwa kwa ajili ya kusikilizwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment