07 June 2012

Simba ziarani Kanda ya Ziwa Juni 16


Na Zahoro Mlanzi

KLABU ya Simba, imepanga kufanya ziara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kuanzia Juni 16 na 17 mwaka huu yenye lengo la kusherehekea kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Mbali na hilo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Kilimanjaro Lager, imepanga kuikabidhi timu hiyo basi jipya la kisasa siku ya Simba Day, ambayo hufanyika kila mwaka Agosti 8.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kutangaza rasmi ziara hiyo, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Rage alisema ziara hiyo ni maalumu kwa ajili ya kupeleka kombe walilotwaa kwa mashabiki wao wa Kanda ya Ziwa.

"Tutaanzia Shinyanga Juni 16 ambapo tutacheza na Toto African na kisha kwenda Mwanza nako tutacheza na timu moja kutoka Uganda, ambapo mazungumzo yanaendelea na ikiwa tayari tutaitangaza," alisema Rage.

Alisema mashabiki wa mikoa hiyo watapata fursa ya kufurahia mafanikio ya timu yao kwa msimu uliopita na watashuhudia ushirikiano uliopo kati yao na TBL.

Naye Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema wanaishukuru timu hiyo kwa kuendelea kuwaunganisha pamoja Watanzania kwa mafanikio wanayoyapata na pia kutekeleza yanayopaswa kufanywa katika mkataba wao.

No comments:

Post a Comment