19 June 2012

Simba yamfungashia virago Machaku


Na Zahoro Mlanzi

KLABU ya Simba, imetangaza rasmi kusitisha mkataba wa kiungo wake, Salum Machaku kwa ajili ya maslahi ya klabu na ya mchezaji mwenyewe.

Mbali na hilo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Milovan Cirkovic anatarajia kutua nchini Ijumaa akitokea mapumzikoni nyumbani kwao Serbia, huku wachezaji wa kigeni 'Maproo' nao wanatarajia kuanza kuwasili siku hiyo.


Akizungumza na gazeti hili Makamo Makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa klabu hiyo Ezekiel Kamwaga, alithibitisha kuachwa kwa Machaku kwa kusema kiungo huyo sasa ni mchezaji huru.

"Ni kweli Simba imeamua kusitisha mkataba na Machaku kwa maslahi ya klabu na yake binafsi, hivyo kuanzia hivi sasa huyo ni mchezaji huru na timu yoyote inaweza kumsajili," alisema Kamwaga.

Alipotakiwa kuanisha zaidi sababu za kusitisha mkataba wa kiungo huyo, Kamwaga alisema ni uamuzi wa kawaida ambao wamefanya kama walivyofanya kwa wachezaji wengine na ndiyo maana wameangalia maslahi yake na ya klabu pia.

Mbali na hilo, Kamwaga alisema Cirkovic pamoja na wachezaji Felix Sunzu na Emmanuel Okwi wanatarajia kutua nchini kati ya Alhamisi na Ijumaa ambapo moja kwa moja watajiunga na wenzao walioko kambini.

Akizungumzia suala la kambi, Kamwaga alisema wana wiki ya pili tangu timu hiyo iingie kambini ambapo walianza kwa kuingia 'gmy' na jana jioni walitarajia kuanza mazoezi ya uwanjani kwenye viwanja vya Sigara, Dar es Salaam.

Alisema katika mazoezi hayo ndipo watakapoonekana wachezaji wao wapya waliowasajili msimu huu kwa ajili ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Kagame ambalo linatarajiwa kuanza rasmi Julai 14, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment