19 June 2012
Wazee Yanga wawajia juu wakorofi *Mwape apewa mkono wa kwakheri
Na Elizabeth Mayemba
WAZEE wa Kamati ya Muafaka ya Yanga wamewajia juu baadhi ya wanachama wa klabu hiyo ambao walikwenda kumtolea lugha chafu Seif Ahmed 'Magari', ambaye amekuwa msaada mkubwa kwa timu yao baada ya kufanikisha zoezi zima la usajili yeye pamoja na mfanyabiashara Abdallah Binkleb, ambaye amejitosa katika kinyang'anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana Katibu wa Wazee hao, Ibrahim Akilimali alisema tayari wafanyabiashara hao walisusia kufanya usajili huo, lakini walitumia busara zao na kuwabembeleza ili waendelee na kazi hiyo.
"Kuna wanachama watatu pamoja na kiongozi mmoja wa Kamati ya Utendaji ambao bila aibu walikwenda kwa Seif na kumtolea lugha chafu, hali ambayo ilisababisha asusie kazi hiyo yeye pamoja na wenzake lakini ikabidi tuwaangukie ili waendelee na tunashukuru Mungu walituelewa wazee wao," alisema Akilimali.
Alisema baada ya kukamilika kwa utaratibu mzima wa uchaguzi watachukua hatua kali kwa wanachama hao wakorofi, kwani wanalenga kuipeleka pabaya timu yao hasa katika kipindi hiki ambacho wanakabiliwa na michuno ya Kombe la Kagame na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Katika hatua nyingine, Wazee hao wameazimia kulifuta tawi la Uhuru na kuwataka wanachama wake wakajisajili kwenye matawi mengine kwani tawi hilo lipo kwa ajili ya kueneza migogoro.
"Uanachama hatuwezi kuwafuta isipokuwa wakajisajili kwenye matawi mengine, tutalisimamia na kuhakikisha linafutwa kabisa," alisema.
Katika hatua nyingine uongozi wa klabu hiyo umemfungashia virago mshambuliaji wake, Mzambia Davies Mwape hivyo si mchezaji wao tena.
"Mwape tumemalizana naye hivyo si mchezaji wa Yanga tena, tunaliweka wazi hilo," alisema Katibu Mkuu wa Yanga Selestine Mwesigwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment