27 June 2012

Ratiba ukusanyaji maoni Katiba Mpya yatolewa


 Na Reuben Kagaruki

TUME ya Mabadiliko ya Katiba, inatarajia kuanza kufanya mikutano na wananchi wa mikoa nane kuanzia Julai 2-30 mwaka huu ili kukusanya maoni yao.

Mikoa hiyo ni Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga. Katika Mkoa wa Dodoma, tume itaanza na Wilaya ya Bahi.


Kwa upande wa Kagera, tume itaanza na Wilaya ya Biharamulo, Manyara (Mbulu), Pwani (Mafia), Shinyanga (Kahama), Tanga (Lushoto). Upande wa Zanzibar, tume itaanza katika Mkoa wa Kusini Unguja Wilaya ya Kusini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na tume hiyo Dar es Salaam jana, inasema maadalizi yote yamekamilika pamoja na kuandaa ratiba, kuisambaza katika mikoa na Wilaya husika.

Imesema wajumbe wa tume na watumishi wa Sekretarieti, wamejigawa katika makundi saba ambapo la kwanza litafanya mikutano katika Mkoa mmoja isipokuwa kundi moja ambalo litafanya katika mikoa miwili ya Kusini Unguja, Kusini Pemba.

“Tume inawaomba wananchi kuhudhuria mikutano ambayo tutaifanya na kushiriki kikamilifu kutoa maoni kwa uwazi, uhuru na utulivu,” ilisema taarifa hiyo.

1 comment:

  1. NI VEMA WABUNGE/WAWAKILISHI/TAASISI ZA KISERIKALI NA ZISIZO ZA KISERIKALI ACHIENI TUME IFANYE KAZI ZAKE TUACHE KUPOTOSHA WATANZANIA TUMECHOKA SERIKALI IWAJIBIKE

    ReplyDelete