25 June 2012

Padri Mapunda aihadharisha CCM


Goodkuck Hongo na David John

UGUMU wa maisha unaowakabili Watanzania wengi ni kielelezo kuwa nchi ipo katika hali mbaya hivyo nafasi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuendelea kutawala ipo mashakani.

Padri Baptiste Mapunda ambaye pia ni Mkurungenzi wa Shirika la Farijika la Afrika Mashariki, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akitoa mahubili kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Kalori Lwanga, lililopo Yombo, wilayani Temeke.

Alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na utajiri mwingi unaoweza kuchochea maendeleo ya haraka kijamii na kiuchumi.

Aliongeza kuwa, mfumuko wa bei katika bidhaa mbalimbali, unachangia kuumiza wannchi na kuongeza kuwa hivi sasa, wakazi wa Mbinga, mkoani Ruvuma, hawanywi chai asubuhi kwa sababu bei ya sukari ni kubwa wakati inazalishwa nchini.

“Katika nchi za Kenya na Zambia, vyama tawala viliondolewa madarakani kwa sababu ya kushindwa kuwajibika kwa wananchi, ipo siku CCM nayo itaondoka madarakani, anayetawala milele ni Mungu pekee kama itashindwa kuwajali wananchi wake.

“Propaganda ndani ya nchi yetu zitatufikisha pabaya, wenye mamlaka pamoja na dola, wote wanakandamiza wananchi maskini wanaodai haki zao, Ulaya watu wakigoma wanatekelezewa madai yao tena kwa wakati,” alisema Padri Mapunda na kuongeza kuwa, nchi imefika pabaya ndio maana hata makanisa yanachomwa moto.

Alisema hakuna sababu ya vyombo vya usalama kumdanganya Rais Jakaya Kikwete kuwa hali ya maisha kwa Watanzania ni nzuri badala yake wamweleze ukweli juu ya umaskini uliopo.

“Leo hii ukimuuliza mtoto anapenda kuwa nani, atakwambia angependa kuwa fisadi, watu wachache ndio wanaoitafuta nchi bila kukemewa na viongozi wa dini wamekaa kimya bila kusema ukweli.

“Msingi mzima wa bajeti umewalenga watu matajiri na kuwaacha maskini, huu ndio ukweli kama kuna watu wa vyombo vya dola humu kanisani nendeni mkamweleze Rais Kikwete, mimi ni shuhuda wa Mungu nitaendelea kusema ukweli,” alisema.

Aliongeza kuwa, haiwezekani Tanzania iingie shimoni kwa sababu ya watu wachache wanaotafuta rasilimali za nchi na kusisitiza kuwa, amani gani iliyopo katika jamii wakati kikundi cha watu wenye kiburi wanaweza kuliangamiza Taifa.

Alisema wabunge wote walitoa matusi bungeni, lazima wanyimwe kura katika uchaguzi ujao na kuwaomba waumini, kuiombea nchi ile amani iliyopo iendelee kuwepo na kuwakemea viongozi wachache wanaochangia ugumu wa maisha kwa Watanzania.

“Mimi siropoki wala kukipigia kampeni chama chochote cha siasa bali nahubili neno la Mungu, hata Mtakatifu Yohane Mbatizaji alikatwa kichwa kwa kusema ukweli, mimi nitaendelea kusema ukweli na kitu pekee kitakachoiponya Tanzania ni neno la Mungu,” alisema.

No comments:

Post a Comment