25 June 2012

Dkt. Mwinyi: Mgomo wa madaktari upo *Atangaza kiama cha kuisafisha MSD, ATME watoa tamko



Na Benedict Kaguo, Dodoma

WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt Hussein Mwinyi, amekiri kuwepo mgomo baridi wa madaktari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), na Hospitali ya Rufaa mkoani Dodoma.

Alisema hali katika hospitali nyingine nchini, huduma za matibabu zinaendelea kutolewa kama kawaida.

Akizungumza na Majira mjini Dodoma jana, Dkt. Mwinyi alisema madaktari wachache walioko katika mgomo ni wale wanaofanya mafunzo kwa vitendo katika hospitali hizo lakini wataalamu wa kada nyingine wakiwemo madaktari bingwa, wanaendelea na kazi baada ya kusikia tamko la Serikali la kuwataka kusitisha mgomo.

Alisema Serikali imetoa maagizo kwa Waganga Wakuu wa mikoa na Wilaya kutoa taaarifa haraka kwa vyombo vya dola kwa saababu baadhi ya madaktari walioko kwenye mgomo, wanawatishia maisha wenzao waliopo kazini.

Aliongeza kuwa, Serikali inazidi kusisitiza kuwa mgomo huo ni batili ambapo kesi ya msingi ipo mahakamani.

“Serikali iko tayari kuondoa kesi kuzuia mgomo mahakamani kama madaktari waliogoma watakubali kurudi katika meza ya mazungumzo wakati madai yao yakishughulikiwa.

“Kama wataendelea na msimamo wa kutoheshimu mahakama, hatua za kisheria zitachukua mkondo wake kwani kwa kiwango kikubwa Serikali imetekeleza madai yao likiwemo la kuwaondoa Watendaji Wakuu wa Wizara akiwemo Waziri, Naibu wake, Katibu Mkuu pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali,” alisema.

Aliwataka madaktari kuipa muda Serikali ili iweze kutekeleza madai yao badala ya kugoma hivyo kukamisha utendaji kazi wa Wizara.

Dkt. Mwinyi alisema, hivi sasa kuna kazi kubwa ya kuisafisha Bohari Kuu ya Dawa (MSD), ambayo ilikumbwa na kashfa katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Alisema kama ataendelea kupata ushirikiano ni wazi kuwa Wizara hiyo itakuwa na mikakati madhubuti ya kuondoa kasoro zilizopo.

Wakati huo huo, Mwandishi Heri Shaaban anaripoti kuwa, Chama cha Tiba Asili nchini (ATIME), kimewataka madaktari waliogoma, warudi kazini kwani mgomo huo unaathiri uchumi wa nchi.

Tamko hilo limetolewa Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa chama hicho Bw. Juma Peleu, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema kama mgomo huo utaendelea, uchumi wa nchi utashuka kutokana na wazalishaji kukosa matibabu. “Uchumi wa nchi hii unatokana na wazalishaji ambao ni wananchi sio Serikali,” alisema Bw. Peleu.

Aliongeza kuwa, asilimia kubwa ya watendaji serikalini hawatibiwi nchini bali Watanzania maskini ndio wanaotibiwa katika hospitali za ndani hivyo aliwaomba wasitishe mgomo na kukubali kukaa mezani ili madai yao yaweze kufanyiwa kazi na Serikali.

“Hivi sasa sio muda muafaka wa kufanya mgomo, naomba wasitishe wakati Serikali ikiendelea kutafuta muafaka wa madai yao,” alisema.

Mwenyekiti wa ATIME, Bw. Simba Simba, alitoa wito kwa viongozi wa madaktari kukutana na Serikali wakiwa kazini badala ya kuweka rehani roho za Watanzania kwa kukosa tiba.

Aliiomba Serikali kuunda Mfuko wa Afya ambao utatumika kuchangisha fedha za kushughulikia matatizo ya madaktari ili yasijirudie tena na kuweka taswira mbaya nchini.





No comments:

Post a Comment