26 June 2012

Milovan atua na mbinu mpya Simba *Vifaa vipya hadharani leo



Na Elizabeth Mayemba

KOCHA Mkuu wa Simba Mserbia Cirkovik Milovan tayari amewasili nchini usiku wa kuamkia jana, na leo ataanza rasmi mazoezi kwa timu yake kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza Julai 14, mwaka huu.

Kikosi cha Simba kilitarajiwa kuwasili Dar es Salaam jana usiku kikitokea Kanda ya Ziwa ambapo walikwenda kufanya ziara ya kutembeza kombe lao la Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo pia walicheza mechi mbili za kirafiki kati ya Toto African ya Mwanza na kushinda 2-0 na The Express ya Uganda walitoka sare ya bao 1-1.

Akizungumza kwa simu jana akiwa njiani kuja Dar es Salaam, Msemaji wa klabu hiyo Ezekiel Kamwaga alisema kocha wao tayari amewasili akitokea mapumzikoni kwao Serbia hivyo leo ataanza program yake ya mazoezi kwenye Uwanja wa Sigara Chang'ombe Dar es Salaam, ambapo ameahidi kuwapa mbinu mpya za ushindi wachezaji wake

"Leo vifaa vyetu vipya titakuwa hadharani hivyo mashabiki watapata fursa ya kuwaona kwenye mazoezi huku tukiendelea kuwasubiri wachezaji wetu wa nje ya nchi, tunataka katika michuano ya Kagame timu yetu iwe tishio," alisema Kamwaga.

Alisema mshambuliaji wao Emmanuel Okwi ambaye alikuwa kwao Uganda anatarajiwa kuwasili nchini kesho akiwa na mchezaji mwingine mpya ambaye atasajiliwa na timu yao kwa ajili ya msimu huu.

Kamwaga alisema mechi mbili za kirafiki walizocheza kanda ya Ziwa kwa kiasi kikubwa zimewasaidia kuelekea katika michuano ya Kombe la kagame, hivyo kocha naye akitaka mechi ya majaribio atapendekeza kwa uongozi ili atafutiwe timu lengo likiwa ni kuwajaribu  wachezaji wake wapya.

Msemaji huyo aliwataka mashabiki wao wawe wa tulivu kipindi chote ambacho timu yao ipo katika maandalizi ya Kagame na Ligi Kuu Tanzania Bara, ili waweze kuwapa raha katika michuano inayowakabili.

Mbali ya Simba timu nyingine zitakazoshiriki Kombe la Kagame ni Yanga na Azam FC ambazo zote zimeanza maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo.

No comments:

Post a Comment