01 June 2012
Malkia wa Tabata 2012 kupatikana leo
Na Mwandishi Wetu
MASHINDANO ya kumsaka 'Malkia wa Tabata' Miss Tabata 2012, yanatarajia kufanyika leo katika Ukumbi wa Da’ West Park Tabata, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana mratibu wa mashindano hayo, Joseph Kapinga alisema licha ya kumsaka Malkia huyo pia kutakuwa na burudani ya muziki kutoka kwa bendi za Mashauzi Classic na Mashujaa.
Mratibu huyo alisema mshindi wa kwanza katika kinyang'anyiro hicho atapewa sh. 500,000 na king’amuzi ambayo imelipiwa miezi sita yenye thamani ya sh. 800,000 iliyotolewa na Multichoice.
Alisema mshindi wa pili atapata sh. 500,000, wa tatu sh. 350,000 wakati wa nne na watano kila moja atapata sh. 200,000.
Kapinga alisema warembo watano wataiwakilisha Tabata kwenye mashindano ya Miss Ilala 2012.
Mratibu huyo alisema warembo wengine watakaoingia 10 bora, kila moja atapata sh. 100,000 wakati waliyosalia watapata sh. 50,000 kila moja.
Kapinga alisema mashindano hayo pia yatatumika kwa ajili ya kusherehekea miaka 10 tangu kuasisiwa kwa Miss Tabata.
“Mashindano ya mwaka huu si ya kukosa, kwani yatakuwa ni ya aina yake ikizingatiwa kwamba yatatumika kusherehekea miaka 10 tangu kuanza kuandaa Miss Tabata,” alisema Kapinga.
Alisema warembo waliyowahi kushinda mataji mbalimbali ya mashindano hayo, pia wamealikwa kusherehekea miaka 10 ya Miss Tabata.
Mratibu huyo alisema mashindano hayo yamedhaminiwa na Dodoma Wine, Redd's, Integrated Communications, Fredito Entertainment, Multichoice Tanzania, Screen Masters, Kitwe General Traders, Step In Electronics, Brake Point, Atriums Hotel na Lady Pepeta.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment