29 June 2012

Kizimbani kwa matumizi mabaya ya ofisi


Na Rehema Mohamed

WATUMISHI wawili wa Ofisi ya Bodi ya Wataalamu wa Manunuzi, jana wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na makosa mawili likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka.



Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, watumishi hao Mkurugenzi Mkuu Bw. Clemence Tesha na Ofisa Rasilimali Watu Bi. Winfrida Igogo, walitenda kosa hilo Juni 22,2010.

Mbeye ya Hakimu Bw. Faisal Kahamba, wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bi. Salha Abdalah na mwenzake Bi. Sofia Gura, walisema washtakiwa walimuajiri Bw. Amani Ngonyani, katika shunguli za manunuzi wakati hana cheti cha taaluma hiyo na usambazaji.

Walidai Bw. Ngonyani aliajiriwa kama Meneja Mwendesha Biashara wa bodi hiyo kinyume cha sheria.

Katika shitaka la pili, washtakiwa hao wanadaiwa Juni 22,2010 kwa pamoja walimuajiri Bw. Ngonyani katika nafasi hiyo wakati hajasajiriwa kama Mtaalamu wa Manunuzi na Usambazaji.

Shtaka la tatu linamkabili Bw.Ngonyani ambaye anadaiwa Juni 22,2010 jijini Dar es Salaam, kwa makusudi alikubali ajira katika nafasi hiyo akijua hajasajiriwa kama Mtaalamu wa Manunuzi na Usambazaji.

Washrakiwa wote walikana kutenda makosa hayo na wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ambayo ni wadhamini wawili ambao walisaini hati ya dhamana ya sh. milioni 10 kila mmoja. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 26 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment