29 June 2012

Dkt. Shein: Muungano utaendelea kudumu




Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, amesema Muungano uliopo utaendelea kudumu ambapo wananchi wenye maoni kuhusu jambo hilo, waisubiri Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili watoe maoni yao..

Dkt. Shein aliyasema hayo Zanzibar jana wakati akifungua mkutano wa Wastaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano waliopo visiwani humo na kusisitiza kuwa, Muungano huo utaendelea kuwepo.

Alisema hatomuogopa mtu wala kumvumilia kama ana lengo la kuvuruga amani ya Zanzibar kwani amekabidhiwa nchi ikiwa salama na tulivu hivyo atahakikisha inaendelea katika hali hiyo.

“Nalipongeza Jeshi la Polisi kwa kuzuia vurugu zilizofanywa na Jumuiya ya Uwamsho ambazo ziliwahusisha vijana, nawahakikishia wastaafu kuwa, Serikali inathamini sana jitihada zenu kwa maendeleo ya nchi na tutaendelea kushirikiana,” alisema.

Dkt. Shein aliwahakikishia wastaafu na kusisitiza kuwa, atapunguza changamoto zinazowakabili hali itakaporuhusu kutokana na mchango wao wa kulinda rasilimali na usalama wa nchi.

Alisema askari wastaafu kupitia umoja wao (UMAWA), wanastahili pongezi kutokana na kazi kubwa waliyoifanya wakati wa uchumaji karafuu ulioweza kuongeza malengo ya ununuaji zao hilo.

Aliongeza kuwa, wastaafu hao wana hazina kubwa zinazohitajika kwenye jamii kama elimu na uzoefu kwani unaweza kununua elimu lakini ukashindwa kununua uzoefu.

“Ukitaka uzoefu lazima uende kwa wazoefu ambao kwetu sisi ni wastaafu hivyo naomba mtambue kuwa, Serikali na wananchi bado wanahitaji uzoefu na ushauri wenu katika mambo mbalimbali.

“Nawaomba muelewe kuwa, utaalamu na uzoefu wa fani zenu haumaliziki pale mnapostaafu, bado vitu hivi vinabaki kama hazina ambayo Taifa inauhitaji wakati wote wa maisha yanu,” alisema.

Dk. Shein alisema, hakuna mja anaeweza kuzilipa jitihada zao, lakini kwa kuwa walijitolea kwa nia njema na maendeleo ya Taifa lao, Serikali itathamini jitihada hizo.

Alisisitiza ari ya kujitolea na kutoa wito kwa wastaafu kushirikiana na Serikali katika jitihada za kuhamasisha vijana.

Mwenyekiti wa UMAWA, Bw. Mohammed Ali, alisema jumuiya hiyo imekuwa na msada mkubwa katika kuchochea maendeleo, kutetea masilahi yao pamoja na kupunguza umaskini kwa kuwajengea uwezo kiuchumi na kijamii.

“Sisi tuna uwezo wa kitaalamu na tuko tayari kushirikiana na Serikali ili kuleta maendeleo endelevu, kilio chetu ni ufinyu wa pensheni tunayoipata ambayo haikidhi haja na muda umekuwa mkubwa tangu tuhaidiwe,” alisema.

Alisema wao wanautaka Muungano uliopo udunu, wanautambua na kuufahamu vizuri pamoja na faida zake hivyo waliahidi kuulinda kwa nguvu zote.

Aliongeza kuwa, jumuiya hiyo ina wanachama 536 ambapo fedha za za pencheni wanazolipwa kwa mwezi kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni zaidi ya sh. bilioni mbili.

No comments:

Post a Comment