19 June 2012

Kidunda: Nina nafasi ya kufanya vyema


Na Amina Athumani

MWAKILISHI wa Tanzania katika michezo ya Olimpiki bondia wa ngumi za ridhaa Selemani Kidunda, amesema ingawa amekosa mapambano ya kimataifa bado ana nafasi ya kufanya vyema katika michezo hiyo.

Michuano ya Olimpiki inatarajia kufanyika London, Uingereza Julai 27 mwaka huu ambapo Tanzania itawakilishwa na wanamichezo sita akiwemo Kidunda na wanariadha Zakia Mrisho, Samson Ramadhan, Dickson Marwa na Faustin Musa pamoja na muogeleaji Magdalena Mushi.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kindunda alisema mechi za kirafiki alizocheza makocha wake wamepata nafasi ya kurekebisha makosa yaliyojitokeza na kwamba bado anayo nafasi nzuri ya kufanya vyema kwenye michezo ya Olimpiki.

Alisema hakupata mapambano mengi ya kimataifa kama kama ilivyoshindikana kwenda Botswana na yale yanayoendelea nchini Kenya kutokana na Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT) kukumbwa na ukosefu wa fedha.

Kidunda ambaye kwa sasa yupo Kibaha, Pwani katika kambi iliyopo Shule ya Sekondari ya Filbert Bayi, ananolewa na kocha Zakaria Gwandu pamoja na bondia mmoja kwa ajili ya kumpa sapoti.

Wawakilishi hao wa Tanzania katika michezo Olimpiki wanatarajia kuondoka nchini Julai 8, mwaka huu kwenda kwenye michuano hiyo.

No comments:

Post a Comment