19 June 2012
EBBS yaibua vipaji kibao Dodoma
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
PAZIA la mashindano ya Epiq Bongo Star Search (EBSS) kwa Mkoa wa Dodoma, limefungwa rasmi jana huku vipaji vingi vikiwa vimejitokeza na kuwavutia majaji.
Kilichovutia zaidi ni washiriki wa miaka 16, ambao walionekana kuimba vyema na kuwafurahisha hata kwa washiriki wenzao waliofurika katika Ukumbi wa Royal Village.
Akizungumzia mshindano hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Benchmark Production inayoandaa EBSS, Ritha Paulsen alisema amevutiwa na wingi wa washiriki mkoani hapa, hasa idadi ya washiriki ya wasichana.
Alisema ikiwa ni mara ya kwanza kuruhusu washiriki wa miaka 16 kuingia katika usaili wa EBSS 2012, ameshuhudia hazina kubwa ya vipaji vya washiriki wa umri huo.
Katika usaili huo kulikuwa na washiriki wa aina mbalimbali wakiwemo wanafunzi, wafanyabiashara ndogondogo, vijana wa mitaani na wadau wengine wa muziki.
Kwa kuthamini umuhimu wa akina mama na watoto mshiriki aliyefika kuonesha kipaji chake katika ukumbi huo alipewa nafasi ya kuimba, ili aweze kuwahi kuondoka.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Kampuni ya Mawasiliano ya Zantel ambao ni wadhamini wakuu wa EBSS 2012 Awaichi Mawalla, mbali na kuvutiwa na ushiriki wa vijana waliojitokeza, pia alihamasisha upimaji wa damu kwa kuchangia damu kwa kituo cha damu mkoani Dodoma.
“Kwa kupitia EBSS 2012, tunataka kuwafikia vijana si tu katika muziki bali hata katika kuhamasisha masuala mbalimbali yahusuyo jamii kama vile hili la kuchangia damu na mengineo,” alisema Awaichi.
Washindi watakaopatikana watatangazwa baadaye katika vyombo vya habari. Baada ya Dodoma kwa sasa inafuata Zanzibar Ijumaa ijayo katika eneo la Ngome Kongwe.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment