25 May 2012

Watumishi wa umma kugoma Julai-TUGHE


Na Moses Mabula, Tabora

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya taifa (TUGHE) Bw. Ally Kiwenge ameitaka Serikali itekeleze kwa vitendo ahadi yake ya kupandisha mishahara kwa watumishi wa umma ifikapo Julai Mosi mwaka huu ili kuepusha mivutano baina ya pande hizo mbili.


Bw. Kiwenge alitoa kauli hiyo jana mjini Tabora alipokuwa akizungumza na watumishi wa afya katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora Kitete.

Alisema kwamba, Serikali ni lazima itekeleze ahadi yake hiyo kwa watumishi wake kama ambavyo Rais Jakaya Kikwete alivyoahidi siku ya maadhimisho ya wafanayakazi Duniani Mei Mosi yaliyofanyika mkoani Tanga.

Alisema kuwa, kila mwaka Serikali imekuwa ikitangaza nyongeza hewa ya mishahara kwa watumishi wake hususan wale wa sekta ya afya hali ambayo inafanya watumishi kutokuwa na imani na ahadi za Serikali yao na kupekelekea kufanya kazi chini ya kiwango.

“Chonde chonde mheshimiwa Rais Kikwete ninakuomba ahadi yako iwe ya kweli, sisi hapa tunasubiri tu, ifikapo Julai mwaka huu 'kahela ketu' kawe kameongezeka kwenye akaunti zetu,” alisisitiza Bw.Kiwenge.

“Sisi hatuna ugonvi na Serikali hata kidogo ugonvi wetu ni masilahi duni, lakini 'kamshahara ketu' kakiongezeka' sisi hatuna mgogoro kabisa na Serikali,” alisema Bw. Kiwenge.

Akiwageukia watumishi wa afya Bw. Kiwenge aliwataka wauguzi wote hapa nchini kutoa huduma ya afya kwa wagonjwa kwa moyo wa upendo, huruma na kutowanyanyapaa.

Alisema kuwa, kiapo cha muuguzi ni kuwa na upendo, huruma kwa wagonjwa wanaowahudumia sanjari na kujiupusha na vitendo vinavyokwenda kinyume na viapo vyao vya kazi yao ya uuguzi.

Alisema kuwa, kazi ya muuguzi ni kutoa huduma bora kwa mgojwa anayefika kutibiwa hospitalini na kwamba kwenda kinyume na kiapo cha cha kazi yake ni kutenda dhambi kwa Mungu.

Katibu Mkuu huyo wa TUGHE taifa alieleza kuwa kazi ya mtumishi wa idara ya afya imebeba dhamana kubwa ya usalama wa afya katika taifa, hivyo ni lazima wahakikishe wanatoa huduma kwa jamii isiyokuwa na mashaka wala malalamiko.

No comments:

Post a Comment