Na Elizabeth Mayemba
SIMBA sasa imepania kufanya kweli katika usajili ambapo wanataka kuziba pengo la kiungo wao Patrick Mafisango aliyefariki katika ajali ya gari hivi karibuni, hivyo wameanza mazungumzo na viungo wanne kutoka Kenya na Uganda.
Mbali ya viungo hao, pia klabu hiyo inampango wa kuwasajili washambuliaji Juma Abdallah wa JKT Ruvu na Jerrson Tegete wa Yanga, lengo ni kuwa na timu bora katika michuano ya Kombe la Kagame na Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Akizungumza na gazeti hili jana mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Usajili ya Simba, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake kwa madai wakati wa kuweka hadharani usajili bado, alisema tayari wameanza mazungumzo na viungo watano ambapo wawili kutoka Kenya na wawili wanatokea Uganda, na kwa hapa nchini wameanza mazungumzo na washambuliaji wawili.
"Tutavunja rekodi katika usajili wetu wala hatutaki kukurupuka lengo ni kuwa na kikosi kilicho bora na si bora kikosi," alisema Mjumbe huyo.
Aliwataja viungo hao ambao mmoja wapo ataziba pengo la Mafisango kuwa ni kiungo wao wa zamani Jerry Santo ambaye kwa sasa anachezea Tusker ya Kenya, Salim Kije wa FC Leopard ya Kenya, Owen Kasule na Mike Muchaba wote wa Bunamwaya ya Uganda.
Mjumbe huyo alisema baada ya kamati yao kuorodhesha majina hayo wataanza mara moja kupeleleza rekodi ya mchezaji mmoja mmoja na watakayevutiwa naye watamsajili na kumtangaza moja kwa moja.
Pia kwa wachezaji wazalendo Abdallah Juma hana tatizo lolote ni makubaliano tu, ila Tegete kuna baadhi ya vitu wanamchunguza na wakijiridhisha watamsajili katika kikosi chao.
No comments:
Post a Comment