31 May 2012

Watoto watumikishwa wilayani Mbarali


Na Esther Macha, Mbeya

LICHA ya Serikali kupiga vita ajira kwa watoto hususan wanafunzi bado
tabia hiyo inaendelea kwa wananchi wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya ambapo kundi hilo la watoto limeshindwa kuhudhuria masomo kwa kufanya kazi katika
mashamba mbalimbali wilayani humo.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni wakati mwandishi wa habari hizi
alipotembelea mashamba ya mpunga, vitunguu na nyanya yaliyopo wilayani
Mbarali mkoani Mbeya.

Wakizungumzia ajira hizo wanafunzi hao walisema, wanalazimika kufanya
kazi hizo kwa malipo ya sh. 200 kwa kila 'kijaruba' hata katika muda wa masomo ili kujikwamua kimaisha.

Hatua hiyo ambayo imekuwa ikipigwa vita na vyombo vya habari na vile
vinavyotetea haki za watoto bado wazazi wameendelea kuwaanchia huru
watoto wao, ambao hutoroka shule na kujishughulisha na kazi za vibarua
katika mashamba ya mazao mbalimbali.

Watoto hao waliokutwa katika ajira hizo ni wale wanasoma darasa la
saba na darasa la tano ambao kwa mujibu wao wanalazimika kufanya
vibarua hivyo ili waweze kupata michango ya shule kutokana na wazazi
wao kutokuwa na uwezo wa kuwasaidia.

Walisema, hupewa kazi hizo na wakulima kwa kukwepa gharama kubwa na kuwa wanashindwa kuwapatia vibarua watu wazima ambao huhitaji kiasi kikubwa cha fedha.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Igomelo Bi.Mima Mkiramweni alisema
kuwa tatizo hilo lipo kwa baadhi ya wanafunzi ambao wanakosa mahitaji
kutoka kwa wazazi wao na hivyo hutoroka shuleni ili kufanya kazi hizo.

“Hawa wakulima na wafanyabiashara ambao wanatoa ajira mbaya kwa
watoto kwa kiasi kikubwa wanasababisha kushuka kwa kiwango cha elimu
shuleni hapa, hili si jambo zuri,”alisema Mwalimu huyo.

Akizungumzia kuhusu mrundikano wa wanafunzi darasani Bi. Mkiramweni
alisema, kila darasa lina wanafunzi 100 mpaka 121 hali ambayo
inasababishwa na ukosefu wa vyumba vya madarasa na hivyo kufanya
ufundishaji kwa walimu kuwa mgumu kwa wanafunzi.

Mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Igomelo wa darasa la saba Frank
Mbuna alisema, katika darasa lao wapo wanafunzi 121 hali ambayo inawaathiri katika taaluma zao.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Shule ya Msingi Wilaya ya Mbarali
Bi. Rustika Turuka alisema, kitendo cha wanafunzi kufanya vibarua
kipindi cha masomo ni kibaya kwani kinashusha kiwango cha elimu kwa
watoto wilayani humo.

Bi. Turuka alisema serikali ilikataza ajira mbaya kwa watoto kwa
kuwatumikishwa kwenye mashamba, na kuwataka wazazi wasaidie  kupiga
vita ajira hizo kwa watoto Wilayani humo

No comments:

Post a Comment