04 May 2012
Watakiwa kujenga utamaduni wa kupima ardhi, kumbukumbu
Na Florah Temba, Kilimanjaro
WANANCHI mkoani Kilimanjaro wametakiwa kujijengea tabia ya kupima ardhi na kuweka kumbukumbu kwa njia ya maandishi hatua ambayo itasaidia kuondoa tatizo la migogoro ya ardhi baina ya wanandugu ambalo limekuwa likiyakumba maeneo mengi mkoani humo.
Rai hiyo ilitolewa na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Upimaji Ardhi na Uendelezaji wa Makazi mkoani hapa Bw. Evans Ngolly wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na changamoto wanazokabiliana nazo katika suala la upimaji ardhi kwenye jamii.
Bw. Ngolly alisema utaratibu wa upimaji ardhi katika familia nyingi mkoani Kilimanjaro hauko bayana hali ambayo imekuwa ikisababisha kuzuka kwa migogoro baina ya wanandugu.
Alisema, ni vema wananchi wakajiwekea utaratibu wa kupima maeneo yao na kuweka bayana taarifa kwa maandishi ili kuepuka matatizo ya migogoro ya mara kwa mara isiyo ya lazima katika familia ambayo imekuwa ikichangia kurudisha nyuma jitihada za kujiletea maendeleo.
“Upimaji ardhi kwa familia nyingi hauko bayana, yaani ni kwamba wananchi wengi katika mkoa huu bado wamekuwa na taratibu za upimaji ardhi (Vuhamba) kizamani hawaweki taarifa kwa njia za maandishi na hali hii imesababisha kuwepo kwa migogoro baina ya wanandugu pindi mmoja anapotaka kupima ardhi yake na kupewa hati miliki ambapo kila mmoja huibuka na kusema sehemu hiyo ni yake,”alisema Bw. Ngolly.
Bw. ANgolly alisema changamoto nyingine wanayokumbana nayo ni pamoja na wananchi wengi kutokuwa na uelewa wa upimaji ardhi na kupata hati miliki hali ambayo inawafanya wengi kuogopa kujitokeza kupima ardhi zao.
Kutokana na hali hiyo Meneja huyo aliwashauri wananchi mkoani Kilimanjaro kuona umuhimu wa kupima ardhi ili kuweza kuepuka migogoro ya mara kwa mara ambayo inautesa mkoa huo katika maeneo mengi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment