04 May 2012
Kata za Rablwoo, Kisuma zakabidhiwa mradi wa maji
Na Timothy Itembe, Mara
MBUNGE Rorya mkoani Mara Bw. Lameck Airo amekabidhi mradi wa visima viwili kwa nyakati tofauti uliogharimu sh. milioni 12 ndani ya kata za Rablwoo na Kisumwa jimboni humo.
Akikabidhi visima hivyo jana kwa wananchi Bw.Airo alisema kuwa amelazimika kuwachimbia wananchi wake visima kwa kuwa ni moja ya ahadi aliyoahidi wakati wa kampeni zake.
Mbunge huyo alisema, kwa hali hiyo hana budi kutimiza kutokana na ukame unao ikumba wilaya hiyo wa mara kwa mara na kusababisha kuwepo uhaba wa maji.
Alisema, maji hayo yatawasaidia akina mama na watoto wanaotumia mwendo mrefu kwenda kuteka maji sehemu za mbali hususanimtoni na kwenye visima visivyo salama.
Aidha Bw. Lakairo alifafanua kuwa mradi huo uligharimu sh. milioni 12 chini ya usimamizi wa Shirika lisilo la Kiserikali, Global Resource Alliance.
"Watakao nufaika na mradi huo ni Kata ya Rablwoo, Kijiji cha Buturi na Rablwoo pamoja na kitongoji cha Kitongo na Nyamisingisi vya kijiji cha Kisumwa kata ya Kisumwa," alisema.
Mkurugenzi wa shirika hilo Bi. Ester Raphael alisema kuwa shirika lake linajishugulisha na uchimbaji wa visima virefu na pia linahudumia watoto waishio katika mazingira hatarishi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tarime Bw. John Henjewele ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo alisema kuwa ni wabunge wachache wenye moyo wakujituma kama Bw. Lakairo kwa hali hiyo wananchi wamuunge mkono katika suala zima la maendeleo.
Pia Bw. Henjewele aliongeza kuwa maji hayo yatumiwe bila ubaguzi na ukoo na kamati hiyo ipange bei itakayokubalika ambayo itasaidia kuendesha mradi huo katika matengenezo na mambo mengine yatakayojitokeza.
Aidha, aliongeza kuwa kamati itakayochaguliwa ishirikishe vijana wa shule zilizo karibu watatu kutoka shule za sekondari na watatu kutoka shule za msingi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment