30 May 2012

Wanyange Miss Tanzania watakiwa kuchukua fomu



Na Mwali Ibrahim

WANYANGE wanaotaka kushiriki katika mashindano madogo ya kumsaka mwakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Dunia (Miss World 2012) wameombwa kuendelea kuchukua fomu za kuingia katika kinyang’anyiro hicho na kuzirudisha kabla ya Juni 4 mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Lino International Agency ambayo inaandaa mashindano hayo, Hashim Lundenga alisema wanatarajia kufanya mchujo wa washiriki Juni 5, mwaka huu kwa ajili ya kubakiza warembo 10 watakaowania nafasi ya kushiriki mashindano ya Dunia.

Mashindano hayo ya Dunia yamepangwa kufanyika Agosti 18, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Dongsheng Fitness Center, mjini Ordos, Inner Mongolia, China.

Lundenga alisema utaratibu huo ulisimamishwa kutokana na zuio la serikali na wakati huo, jumla ya warembo 12 walikuwa wamekwishachukua fomu za ushiriki.

Alisema muda wa kufanya mashindano hayo, umekaribia na wanatarajia kuitangaza tarehe mpya hivi karibuni.

Mkurugenzi huyo alisema amefurahishwa na kasi ya uchukuaji na kurejesha fomu, hata hivyo wanahitaji warembo wengi zaidi ili kupata wigo mpana kwa ajili ya kumsaka mrembo atakayewania taji la Dunia, ambalo kwa sasa lina mikononi mwa mrembo kutoka Venezuela, Ivian Sarcos.

“Tunakaribia kufanya mashindano madogo hivi karibuni, hivyo ni wajibu wetu kuwakumbusha warembo wanaotaka kuwania taji hilo kufanya hivyo kabla ya Juni 4, mwaka huu ili kuweza kuingia katika mchakato wa mchujo,” alisema Lundenga.

Alisema mpaka sasa jumla ya nchi 84, zimekwishapata wawakilishi wao kwa ajili ya mashindano hayo. Nchi 32 pamoja na Tanzania bado hazijachagua wawakilishi wao katika mashindano hayo.

Lundenga alisema fomu za kuomba kushiriki zinapatikana katika ofisi za Miss Tanzania za jijini na mawakala wote wa mashindano hayo katika mikoa ya Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment