03 May 2012
Wananchi waitaka serikali kujenga mifereji
Na Florah Temba, Kilimanjaro
WANANCHI wilayani Same mkoani Kilimanjaro wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kujenga mifereji katika barabara inayotoka Ndungu hadi Mamba Myamba ili kupunguza matatizo ya uharibifu wa barabara unaotokea mara kwa mara kwa kusababishwa na mvua.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara wananchi hao walisema ukosefu wa mifereji katika barabara hiyo ni moja ya changamoto inayowakabili katika wilaya hiyo ambapo hutokea madhara makubwa pindi mvua zinaponyesha na kuigharimu Serikali gharama kubwa.
Walisema kuna haja ya Serikali kujenga mifereji katika barabara hiyo ili kuwezesha maji ya mvua kupata mwelekeo badala ya kuingia barabarani.
"Tunaishukuru Serikali kwa kutujengea barabara ya Ndungu Mamba Myamba kwa kuwa sasa inapitika vizuri, lakini tatizo kubwa ni barabara hiyo kukosa mifereji jambo ambalo ni la hatari," walisema.
Walisema ni vyema Serikali ikachukua tahadhari kabla ya maafa kutokea na kusababisha hasara ambayo itaigharimu mabilioni ya fedha ambayo yangeweza kutumika kuendeleza sekta zingine.
Akizungumzia hali hiyo ya ukosefu wa mifereji katika barabara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw.Leonidas Gama, alisema suala la mifereji katika barabara hiyo ni la muhimu ili kuilinda isiharibike.
Aliagiza Halmashauri ya Wilaya ya Same kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kufuatilia suala hilo na kuhakikisha mifereji inajengwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment