03 May 2012
Viongozi wa klabu za waandishi wa habari wapewa changamoto
Na Damiano Mkumbo, Singida
VIONGOZI wa klabu za waandishi wa habari nchini wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili jamii iweze kunufaika na mchango kwa maendeleo ya taifa.
Mwito huo ulitolewa na Ofisa Programu, Mafunzo na Utafiti wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Bw.Ernest Kambili, wakati akifunga mafunzo ya wiki moja ya uandishi wa habari za uchunguzi yaliyomalizika mjini Singida hivi karibuni.
Bw.Kambili alisema klabu hizo ni nyeti kwa kuwa zinashughulikia mambo yanayohusu watu na shughuli zao katika maisha ya kila siku, hivyo viongozi wawe na dhana ya utekelezaji wa wajibu wao kidemokrasia.
"Fanyeni kazi zenu kwa ushirikiano na kujali mipaka ya madaraka kulingana na katiba zenu, kwani hakuna anayejua zaidi kuliko mwingine na kuwa na mawazo ya kujenga bila kubahatisha mambo," alisema.
Alieleza kuwa viongozi si mameneja kwani vilabu pia si makampuni binafsi, isipokuwa ni mali ya wanachama wote ambao wanapaswa kushirikiana pamoja na kuviendeleza kwa faida yao na taifa kwa ujumla.
"Tekelezeni wajibu wenu bila upendeleo na kuchapa kazi kwa bidii kutokana na dhamana mliyokabidhiwa katika kufikia viwango vizuri na mafanikio ya klabu zenu kama zingine chache zilizo mfano mzuri," alisema.
Akizungumza kuhusu mpango mkakati wa UTPC alisema kuwa malengo ya kutoa mafunzo mbalimbali kwa wanachama ili waweze kujengewa uwezo wa kuongeza maarifa na ujuzi na kutoa vifaa vitakavyowasaidia kufanya kazi zao kulingana na mabadiliko ya sasa.
Naye Mkufunzi katika mafunzo hayo, Bw. Nyaronyo Kichere, alisisitiza juu ya umuhimu wa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari za uchunguzi kwa kuandika ukweli uliojificha.
Bw.Kichere ambaye ni mwandishi mkongwe na wakili wa kujitegemea, alieleza kuwa mwandishi ni jicho la jamii lazima afanye kazi yake kwa ajili ya masilahi ya taifa bila kuathiriwa na rushwa, urafiki, undugu na itikadi za siasa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment