24 May 2012
UPDP walaani vurugu zilizotokea Rufiji
Na Rehema Maigala, Pwani
MWENYEKITI wa Chama cha Siasa UPDP Mkoa wa Pwani Bi. Asha Chuma amelaani uzembe wa Serikali kufumbia macho mauaji na uharibifu wa mali uliotokea hivi karibuni Ikwiriri wilayani Rufiji.
Akizungumza na gazeti hili jana Bi. Chuma alisema kuwa kitendo hicho kinaonyesha wazi kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inafumbia macho watumishi waovu na wasioelewa sheria za kazi zao.
Alisema kuwa, hali hii inaonyesha wazi kuwa CCM na Serikali bado inasimamia sera chakavu ya ardhi na kumilikiwa na chama kinachounda serikali hasa pale serikali husika inapokuwa haina uzalendo wala uadilifu.
"Serikali ilitakiwa kutolea macho suala hilo kwani kitendo cha mauaji na uharibifu wa mali huku Ikwiriri kinaonyesha wazi kuwa Serikali haiko macho na mambo yanayoendelea kutendeka," alisema Bi.Chuma.
Hata hivyo wananchi wa mkoa huo walikaa kikao cha pamoja na Mkuu wa Operesheni Maalum Jeshi la Polisi nchini Bw. Simon Siro walikaa pamoja na kuaswa kutokufanya vurugu ikiwemo kuweka maazimio mbadala.
Pia walianzimia wafugaji warudi katika mipaka yao na wasivuke kuingia maeneo ya wakulima na viongozi wasiotekeleza majukumu yao ipasavyo wawajibishwe.
Maazimio mengine ni kuhusu viongozi, polisi na watendaji wengine wa Serikali wanaojihusisha na rushwa wachukuliwe hatua, wafugaji waliohusika katika mauaji ya wakulima Bw. Shamte Kawangala (80) wakamatwe na wafikishwe mahakamani.
Kamanda alisema kuwa, wananchi 53 waliokamatwa na kufikishwa mahakamani mashtaka yao yachunguzwe kwa kina na wale wasiohusika waachiwe na watakaobainika kuhusika sheria ichukue mkondo wake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment