24 May 2012
Timu ya taifa ya riadha Zanzibar yakabiliwa na ukata
Na Mwajuma Juma, Zanzibar
TIMU ya Taifa ya Riadha ya Zanzibar inayojiandaa na mashindano ya vijana ya Afrika Mashariki na Kati inakabiliwa na ukata mkubwa ikiwemo vifaa vya kufanyia mazoezi.
Timu hiyo inajiandaa na mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar Es Salaam juni 7-8 mwaka huu.
Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wachezaji wanaounda timu hiyo, walisema kuwa hadi sasa timu hiyo mbali ya kufanya mazoezi lakini haina huduma yoyote inayopatiwa kuanzia kwa wachezaji hata viongozi.
Wachezaji hao walisema kwamba pamoja na kuwa mchezo wa riadha unailetea sifa nchi, lakini umewekwa nyuma kiasi ambacho wanavunjika moyo.
“Sisi tunajiandaa na mashindano makubwa lakini hadi muda huu hatujawekwa kambini, na wala hakuna kiongozi hata mmoja aliyepita angalau kutuwekea ahadi”, alisema Nasria Hashim.
Nasria ambae ni mwanariadha anayetambulika kimataifa alisema kuwa wamekuwa wakifanya mazoezi kwa kujitegemea wenyewe wakikosa hata maji.
“Hivi sasa ninavyozungumza na wewe tumemaliza mazoezi tunasubiri mgao wa maziwa wa wachezaji wa KMKM”, alisema Ipyana Mwakabana.
Sambamba na hilo wachezaji hao walisema kuwa mbali na kukosa huduma hizo pia timu hiyo inakosa daktari wa kuwatibu wanapopatwa na matatizo na kufikia hatua ya kujitibu wenyewe binafsi.
“Sio lazima tupewe kila kitu lakini vitu viwili ni lazima ikiwemo daktari na maji, tumekuwa kama watoto yatima tunaomba tuangaliwe kwa jicho la huruma”, alisema Hassan Khamis.
Nae Mwenyekiti wa chama cha Riadha Zanzibar Khamis Tawakal alithibitisha kuwepo kwa ukata huo ndani ya timu hiyo, ingawa alisema kuwa bado hawajatangaza kikosi ambacho kitashiriki michuano hiyo.
Alisema kwamba wapo wachezaji ambao wanafanya mazoezi lakini bado hajapokea majina rasmi kwa wale ambao watashiriki mashindano hayo.
“Tuna wachezaji zaidi ya 25 tumewakusanya ambao tunawaandaa lakini ni kweli timu ipo katika maandalizi mabaya na haya yote yametokana na ukosefu wa fedha pamoja na wafadhili”, alisema Tawakal.
Timu ya Taifa ya Zanzibar ya Riadha inatarajiwa kuondoka nchini Juni 5, mwaka huu kwa ajili ya kushiriki michuano hiyo ambayo inashrikisha nchi za Afrika Mashariki na Kati, zikiwemo Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda, Zanzibar na wenyeji Tanzania Bara.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment