22 May 2012

Taa ya chemli yaua Morogoro


MKAZI wa maeneo ya Kasanga wilayani Morogoro Mkoa wa Morogoro Bw. Lucas Robert (48) amefariki dunia mara baada ya kulipukiwa na taa ya chemli aliyokuwa akiiwasha.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Bi. Adolphina Chialo tukio hilo lilitokea Aprili 17, mwaka huu, majira ya saa 12.45 alasiri maeneo ya Kasanga na kusababisha kifo chake wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya mkoa.


Hata hivyo, Kamanda huyo alisema chanzo cha tukio hilo kinachunguzwa zaidi.

Wakati huohuo Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linaendelea kumfanyia uchunguzi utingo wa gari anaedaiwa kulishwa chakula chenye madawa ya kulevya huko maeneo ya Mikumi wilayani Kilosa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro Bi. Adolphina Chialo tukio hilo lilitokea Mei 20, mwaka huu, majira ya saa 10.00 jioni huko maeneo ya Mikumi Wilaya ya Kilosa.

Kamanda Chialo alisema Bw. Ramadhani Salumu (33) ambaye ni dereva wa gari lenye namba za usajili T 509 ARS aina ya Scania Trela, alikuwa akitokea nchini Zambia kuelekea jijini Dar es Salaam na alitoa taarifa kuwa utingo wake aliyefahamika kwa jina Bw. Saimon Mashaka (21) amelishwa chakula kinachodaiwa kuwa na madawa ya kulevya.

Hata hivyo Kamanda huyo alisema utingo huyo amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro na uchunguzi zaidi unaendelea kuhusiana na tukio hilo.

No comments:

Post a Comment