Na Zahoro Mlanzi
MSHAMBULIAJI wa timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Demokrasi ya Congo (DRC) raia wa Tanzania, Mbwana Samatta amezidi kuonesha cheche zake baada ya kuifungia bao timu yake katika ushindi wa mabao 2-0, walioupata dhidi ya El Merreikh ya Sudan katika mechi ya Klabu Bingwa Afrika.
Mechi hiyo iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Kibassa Maliba mjini Lubumbashi, iliifanya timu hiyo ianze vizuri hatua ya 16 bora ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi za klabu Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtandao wa klabu hiyo juzi, ilieleza kwamba Samatta alifunga bao hilo dakika ya 22 kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Tressor Mputu na kumfanya nyota huyo kuiongoza timu hiyo mpaka kipindi cha kwanza kikimalizika kuwa mbele kwa bao 1-0.
TP Mazembe inayonolewa na Kocha Lamine Ndiaye, ilitawala mechi hiyo katika kipindi cha kwanza licha ya wageni wao pia kuonesha cheche zao hasa kwa shambulizi walilofanya dakika ya 39 lakini kutokana na uwezo wa kipa wao, Kidiaba aliokoa mpira uliokuwa ukienda langoni mwake.
Nahodha Mputu aliifungia timu yake bao la pili dakika ya 70 kwa shuti kali nje ya eneo la hatari, lililokwenda moja kwa moja wavuni na kuihakikishia timu hiyo kuibuka na ushindi huo nyumbani.
Safu ya ushambuliaji ya Mazembe iliundwa na wakali kama MPUTU, Given Singuluma, Kalaba na Samatta ambayo ndiyo safu iliyocheza mechi ya kwanza ya michuano hiyo dhidi ya Power Dymanos ya Zambia katika sare ya bao 1-1.
Katika mechi hiyo, bao la kusawazisha la TP Mazembe lilifungwa na Samatta lakini mechi ya marudiano ambayo TP Mazembe ilishinda hakucheza kutokana na kuwa majeruhi.
Mazembe itakuwa na kibarua kigumu katika mechi yao ya marudiano kwa kusafiri mpaka jijini Khatoum, katika mechi ya marudiano ambapo wakishindwa kwenye mechi hizo za 16 bora, watacheza katika Kombe la Shirikisho ambapo kwa hapa nchini Simba ndiyo timu pekee inayoiwakilisha katika michuano hiyo.
Samatta kabla ya kujiunga na Mazembe alikuwa akiichezea Simba, ambaye alijiunga nayo katikati ya msimu wa mwaka jana kwa uhamisho ambao uliweka historia kubwa nchini kwa kununuliwa kwa zaidi ya milioni 150.
No comments:
Post a Comment