02 May 2012

Simba waiendea Yanga Visiwani

Na Elizabeth Mayemba

TIMU ya soka ya Simba jana wamekwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga, unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi ijayo.

Simba juzi walikuwa na mechi ngumu ya Kombe la Shirikisho (CAF), dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan ambapo walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0. Kwa ushindi huo Simba katika mechi ya marudiano wanahitaji sare ya aina yoyote na wapinzani wao ili wasonge mbele.

Wawakilishi hao katika michuano ya CAF wapo katika harakati za kuwania ubingwa wa Bara ambao nafasi hiyo pia inawaniwa na Azam FC.

Simba wanaomba Mungu, Azam wapoteze mchezo mmoja au kutoa sare katika mechi mbili walizobakiza, kwani endapo Azam watashinda mechi zake zote mbili ubingwa wa Simba utakuwa mikononi mwa Yanga.

Akizungumza Dar es Salaam juzi mara baada ya mchezo wao na Al Ahly Shandy kumalizika, Kocha Mkuu wa Simba Milovan Cirkovic alisema sasa akili zake anaelekeza kwenye mchezo wao wa Jumamosi.

"Mechi inayokuja mbele yetu ni ile ya Ligi Kuu dhidi ya Yanga hivyo sasa hivi akili zetu tunaelekeza huko, lengo likiwa ni kuibuka na ushindi, tunajua mchezo utakuwa mgumu kutokana na historia iliyopo kwa timu hizo mbili kila zinapokutana," alisema Milovan.

Alisema baada ya mechi hiyo ya kihistoria kumalizika, atageukia kwenye maandalizi ya mechi yao ya marudiano ya Kombe la Shirikisho (CAF), dhidi ya Al Ahly Shendi kwani ni mechi muhimu sana kwao.

Milovan alisema timu yake kwa sasa ipo vizuri hivyo anaimani itafanya vizuri zaidi katika michuano mbalimbali inayowakabili.






No comments:

Post a Comment