23 May 2012

Polisi wakamata bunduki 4, risasi 436


Na Thomas Dominick

JESHI la Polisi mkoani Mara, limefanikiwa kukamata bunduki nne aina ya Short Gun, SMG na risasi 436 katika kipindi cha wiki mbili baada ya kuwakamata watuhumiwa nane wanaodaiwa kufanya uhalifu na uwindaji katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.


Akizungumza na Majira, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Robert Boaz, alisema jeshi hilo lilipata taarifa za mkazi wa Kijiji cha Bisarara, wilayani hapa Bw. Marwa Makoba (40), kuwa anamiliki silaha hivyo walikwenda kijijini hapo ili kumkamata.

“Baada ya kumkamata, tulifanya upekuzi nyumbani kwake na kupata silaha mbili aina ya SMG na risasi 228, alipofikishwa kituoni tulifanya naye mahojiano kwa kina na kusema anashirikiana na wenzake watano,” alisema Kamanda Boaz.

Aliongeza kuwa, Bw. Makoba aliwataja wenzake kutoka mikoa mbalimbali ambao wakati huo walikuwa mjini Mgumu ndipo polisi walikwenda eneo hilo na kuwakamata.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni, Bw. Fares Nazareti (37), Bw. Erasto Chubwa (46), wakazi wa Bukombe Geita, Magina Bathromeo (36) na Yohana Godfrey (30), wakazi wa Urambo Tabora, Bw. Japhet Bua (28) na Bw. Amosi Kagoma, wakazi wa Kibondo, mkoani Kigoma.

“Tulipofanya nao mahojiano, Bw. Kagoma alikubali kutupeleka nyumbani kwao Kibondo na kuonesha SMG moja, mwingine Bw.  Godfrey alitupeleka Tabora na kuonesha silaha nyingine,” alisema.

Kamanda Boaz alisema, katika tukio jingine ambalo lilitokea Mei 20 mwaka huu, mtu aliyejulikana kwa jina la Bw. Keringo Samara (30), baada ya kupekuliwa nyumbani kwake alikutwa na risasi sita za SMG ambapo jeshi hilo linaendelea kumuhoji ili kujiridhisha kama anaimiliki kihalali.

No comments:

Post a Comment