23 May 2012

Waliovamia maeneo ya wazi kuondolewa


Na Grace Ndossa

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, inaendelea kufanya ukaguzi katika maeneo yote ya wazi ili kuhakikisha waliovamia maeneo hayo wanaondolewa haraka iwezekavyo.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Bw. Goodluck Ole Medeye aliyasema hayo Dar es Salaam juzi wakati akihojiwa katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na televisheni ya ITV.


Alisema Serikali imeacha maeneo ya wazi kwa ajili ya wananchi kupata sehemu za kukaa wanapopata majanga au hatari yeyote.

“Wizara yangu imeanza kufanya ukaguzi wa maeneo ya wazi katika Wilaya ya Kinondoni ili kuwaondoa wote waliojenga majengo, ukaguzi huu utaendelea mikoani si kwa Dar es Salaam pekee.

“Matumizi ya maeneo ya wazi hayabadiliki, watu wasidanganywe, watu wengi wamejenga hulka ya kuvamia viwanja vya watu, kujenga na kuuza, tukibaini hilo nyumba itabomolewa na muhusika ataondolewa bila serikali kumpa kiwanja kingine,” alisema.

Alisema Wizara hiyo kwa sasa imeboresha nyenzo za kufanyia kazi kwa kutumia teknohama ili waweze kuweka kumbukumbu za ardhi vizuri na kuongeza kuwa, Wenyeviti  na Watendaji wanapaswa kusimamia ardhi zilizopo katika maeneo yao na hawana mamlaka ya kuuza ardhi.


No comments:

Post a Comment