02 May 2012

Mkurugenzi akemea matumizi mabaya ya fedha za miradi

Na Mwajabu Kigaza,
Kigoma.

KAIMU Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya Kigoma vijijini Bw.Adamu Misana
amekemea baadhi ya vitendo vya baadhi ya taasisi, viongozi wa serikali  na mashirika
binafsi kutumia vibaya fedha za miradi kwa kujinufaisha wao badala ya walengwa.

Akifungua mkutano wa wadau wanaohudumia  watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi
wilayani Kigoma Bw. Misana alisema tatizo hilo ni kubwa na linakwamisha jitihada na mikakati ya Serikali katika kupambana na na ongezeko la watoto wa mitaani.

Alisema licha ya mashirika na taassisi mbalimbali  kuomba na kupata fedha kwa ajili
ya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi lakini bado utatuzi wa kutatua
tatizo hilo ni mdogo.

Bw. Misana alisema kuwa tabia ya kuomba miradi ya fedha kwa lengo fulani
nakushindwa kutekeleza kikamilifu kwa maslahi binafsi linawakatisha tamaa
wafadhili ndani na nje ya nchi nakwamba Halmashuri inajipanga kudhibiti tabia
hiyo.

Kwa mujibu wa mratibu katika kituo cha malezi ya watoto yatima cha MWOCACH katika Manispaa ya Kigoma Ujiji Bi. Zainabu Bilandeka alisema ipo haja kwa mashirika na taaisisi hasa za dini na Serikali pia kuweka mbele maslahi ya watoto yatima katika kupata haki za msingi ikiwamo katika bajeti ya serikali kila mwaka.

Bi. Bilandeka alisema ikiwa jamii itaepuka unyanyapaa na kuona tatizo la
watoto yatima si mapenzi yao kutakuwa na tija kubwa ya kuwasaidia kupata haki
za msingi ikiwamo afya, elimu na malazi bora.

Alisema licha ya kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitumia fedha nyingi kwa
starehe zisizo na tija kubwa kwa jamii pamoja na michango ya kiwango kikubwa
katika sherehe lakini wamesahau watoto katika kituo hicho na maeneo mengine
wamekuwa ombaomba bila msaada na hivyo kutoa mwito kwa  mtu mmoja mmoja, vikundi na
mashirika kutembelea vituo vya watoto yatima na kutoa misaada ya hali na mali.


No comments:

Post a Comment