02 May 2012

Mkataba wa Mgambo Ilala umeisha-Mkurugenzi


Na Heri Shaaban

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Bw. Gabriel Fuime, amesema mgambo wote waliokuwa na mikataba ya miezi mitatu imemalizika rasmi juzi, hivyo wametakiwa kurejesha vitendea kazi walivyokuwa wakitumia zikiwemo sare.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Bw. Fuime Aprili 30, mwaka huu, ilieleza kuwa mikataba yao ya ajira imemalizika  rasmi hivyo wanatakiwa kurejesha virungu, pingu na sare ifikapo leo.

Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni siku chache baada ya mgambo hao zaidi ya 150 kugoma kushinikiza kulipwa malipo yao ya zamani ambayo wanadai kuidai Manispaa ya Ilala.

Kwa mujibu wa kiongozi wa mgambo hao (jina linahifadhiwa) alikiri  mkataba wao kumalizika na kila mmoja kutakiwa kurejesha vifaa alivyokuwa akitumia kazini.

Alisema kuwa wao ndio miongozi mwa askari mgambo waliokuwa wakishinikiza manispaa hiyo iwalipe malimbikizo yao ya nyuma, ndio waweze kuingia katika mkataba mpya.

Mgambo hao walisema kuwa jana waliripoti kazini na kukuta tangazo likiwataka mgambo wote ambao walikuwa na ajira ya mda mfupi likiwataarifu mkataba wao kumalizika.

Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Manispaa hiyo Bw.Poll Wanga, alisema mgambo waliokuwa wakitumiwa na manispaa hiyo mkataba wao umemalizika.

No comments:

Post a Comment