17 May 2012

Mara yapitisha bajeti 2012/2013


Na Thomas Dominick
Musoma

MAKADIRIO ya Rasimu ya bajeti ya Mkoa wa Mara kwa kipindi cha mwaka wa fedha
2012/2013,kwani mkoa umeomba kuidhinishiwa zaidi  ya shilingi bilioni 163 sawa na ongezeko la asilimia 22.5 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2011/2012.



Akisoma makadirio ya bajeti hiyo Katika kikao cha Kamati ya Ushauri wa
Mkoa (RCC) Ofisa Mipango wa Mkoa huo, Bw. Nesphory Bwana alisema kuwa
sehemu kubwa ya ongezeko la bajeti hiyo ni mishahara iliyoongezeka kwa
asilimia 44.7. ongezeko hilo la mishahara limetokana na muundo mpya wa
sekretarieti ya mkoa na halmashauri ambapo jumla ya watumishi 152
wataajiriwa na sekretarieti ya mkoa na watumishi 2,607 wataajiriwa na
katika halmashauri za wilaya.


Alisema sh.bilioni 103.456 ni kwa ajili ya mishahara, bilioni 18.238 kwa ajili ya
matumizi mengineyo, bilioni 31.324 kwa ajili ya miradi ya maendeleo na
bilioni 10.443 ni makusanyo ya vyanzo vya ndani

“Pamoja na maombi hayo hapo juu, Mkoa wa Mara unaomba kiasi cha
bilioni 22.573 kama maombi maalumu kwa ajili ya kutekeleza miradi
mbalimbali ya maendeleo kwa Sekretarieti ya mkoa na halmashauri
zake,”alisema Bw. Bwana.

Alisema kuwa bajeti hiyo imezingatia vipaumbele vya wananchi toka
katika ngazi za msingi yaani vijiji, mitaa na kata ushauri toka katika
wizara mama ya OWM- TAMISEMI na wizara za kisekta, wizara ya Fedha,
Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Mabaraza ya Madiwani na kamati za kudumu
halmashauri.

Pia alisema kuwa imezingatia mawazo na mapendekezo ya wadau
mbalimbali, wakiwemo wafanyabiashara, wenye viwanda, sekta ya kilimo,
utalii na wengine wengi.

Awali akifungua mkutano huo Mkuu wa Mkoa huo Bw. John Tuppa aliwaomba
wajumbe na kujadili kwa kina na kutoa maamuzi sahihi yatakayosaidia
mkoa huo na kupewa baraka na wajumbe hao.

“Ukomo wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2012/13 tuliopewa Serikali ni sh.
bilioni 163 ambao ni ongezeko la bilioni 32 ya bajeti ya mwaka jana,
ambapo ongezeko hilo lipo kwenye mishahara, matumizi ya kawaida
imepungua kwa asilimia 40 ambapo katika utendaji kutakuwa na kazi
kweli,”alisema Bw.Tuppa.

Alisema kuwa makusanyo ya ndani ndiyo yatakayookoa mkoa kwani  alidai kuwa hii inatokana na fedha za uendeshaji na maendeleo kuwa ndogo.

No comments:

Post a Comment