14 May 2012
Magereza ziwe vyuo cha maadili kwa wafungwa
Na Darlin Said
KWA nyakati tofauti Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imekuwa ikitoa taarifa juu ya mlundikano wa wafungwa na hali mbaya ya magereza nchini.
Mfungwa ni mtu aliyeadhibiwa kwenda Gerezani baada ya kutenda makosa au uhalifu katika jamii ili kujifunza na kutorudia kosa hilo.
Adhabu hutolewa kisheria na mahakama ambapo hutumikia adhabu hiyo huku akisimamiwa na kurekebishwa tabia zao.
Mfungwa hupokea mafunzo mbalimbali na kupelekea kupata ujuzi katika ufundi, ukulima, ufugaji na fani nyingine nyingi.
Ni tegemeo la serikali na jamii kuwa, mfungwa anamaliza kutumikia kifungo chake awe amebadilika kitabia na kuwa raia mwema anayeweza kushiriki katika kuleta maendeleo ya jamii inayomzunguka.
Kwa kulitambua hilo Chama cha kurekebisha mwenendo wa watu waliomaliza kifungo Tanzania (E.R.S.T) kilianzishwa mwaka 2009 chini ya mwenyekiti Bw.Shafii Kondo ili kuwapatia mafunzo.
Pia, ni kuwaunganisha wafungwa waliomaliza vifungo vyao na kuwarekebisha
tabia zao ili wasiweze kufanya tena uhalifu ambao utawasabishia kurudi tena gerezani.
Lengo lengine ni kutoa elimu katika jamii ili waweze kuwapokea na kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kutumia ujuzi walioupata gerezani.
Vilevile kuhakikisha wanasimamia vema haki za wafungwa zilizosaulika mfano haki ya kupiga kura na ya kukutana na wanandoa wenzao.
Pia kuhakikisha kwamba wanatoa msaada wa kifedha, vifaa na rasilimali ardhi ili iwe changamoto kwa waliomaliza vifungo kujiunga na Taasisi za aina hii ili waweze kujiepusha kujiingiza katika vitendo vya uhalifu.
Ili waweze kufanikisha malengo yao chama kimeanzisha miradi mbalimbali ikiwemo shughuli za kuchana mbao, karakana, ukulima na ufugaji.
Kwa uhalisia tunaona kwamba, katika magereza nchini kuna matatizo ya kisheria yanayopelekea wafungwa kukosa uhuru wao ambayo ni kinyume na haki za binaadamu.
Kwa mfano katika sheria zetu wafungwa hawana haki ya kupiga kura kumchagua kiongozi anayemtaka na pia hawana haki ya kukutana na wanandoa wao ambapo ni kinyume na haki za kibinaadamu.
Serikai inatakiwa kubadili mfumo wa sheria ya magereza kutoka mfumo wa kikoloni ambazo zinaonekana kandamizi kwa wafungwa na kuwanyima haki zao za msingi.
Sheria ziliopo ni za kikoloni wakati wafungwa ni wa kisasa, pia washirikishwe kutoa mawazo yao katika mchakato wa kubadilisha katiba kwani ni haki yao ya msingi.
Katika magereza bado sheria hazijaboreshwa ukilinganisha na sehemu nyingine hali inayopelekea kuwa na matatizo mbalimbali ikiwemo msongamano wa wafungwa.
Magereza mengi yamefurika wafungwa na mahabusu kupita kiasi, huduma za chakula, matibabu na haki nyingine za wafungwa zimekuwa ama haziheshimiwi kabisa au pale zinapoheshimwa ni kwa kiwango cha chini kabisa.
Nionavyo gerezani kuna matatizo mengi ambayo wafungwa wanakumbana nayo ambao aidha yanasabashwa na sheria zilizopo ambayo wafungwa ndio wanayoyafahamu vema kuliko mtu yeyote.
Mfano wafungwa kutoruhusiwa kuwa karibu na waume/wake zao ni tatizo kubwa ambalo linaweza ikapelekea tatito la ushoga gerezani.
Lakini kama kungekuwa na sheria inayoruhusu wafungwa kukutana na wake zao ingesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo hilo na maambukizi ya VVU.
Aidha upande wa serikali itilie mkazo kwa kufanya magereza yawe ni vyuo vya mafunzo ya kuwafanya wafungwa wapate ujuzi mbalimbali na siyo sehemu ya kupata adhabu na unyanyaji .
Tunafahamu na kutambua kuwa magereza siyo hoteli ya kitalii kwa maana hiyo iwe na huduma za kiwango cha juu sana, lakini pia siyo sehemu ya kuwatesa wafungwa na kukataa walau kutambua haki zao za msingi.
Tujifunze kutoka kwa ngugu zetu wa visiwani badala ya kuita magereza wanaita vyuo vya mafunzo hii inasaidia jamii kuwaona wafungwa ni wenzetu ambao wapo mafunzoni.
Kwa upande wa magereza ya watoto, serikali ihakikishe kuwa inawapatia watoto hao elimu bora na wasiwape adhabu kubwa zisizo endana na umri wao.
Kwa kufanya hivyo tunaweza kujenga taifa linalowajali wafungwa ingawaje wametenda makosa au uhalifu katika jamii.
Serikali imetakiwa kuwashirikisha wafungwa katika mchakato mzima wa kupiga kura, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kupata haki ya kukutana na wenzi wao hasa wanapokuwa kifungoni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment