14 May 2012

Mama Tunu Pinda awajaza 'manoti' Taifa Queens



Na Zahoro Mlanzi

BAADA ya kuwa wa pili katika michuano ya netiboli ya Afrika kwa kuifunga Botswana mabao 32-23,Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda ametimiza ahadi aliyoitoa kwa timu ya Taifa ya Netiboli (Taifa Queens) kwa kutoa jumla ya sh. milioni 20.8.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Irene Bwire, ilieleza kwamba Mama Pianda alitoa sh. milioni moja kwa kila mchezaji endapo wangetwaa ubingwa wa kombe hilo ambayo mashindano yake yalimalizika juzi na Malawi kutwaa ubingwa.

Ilieleza Mama Pinda ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kuisaidia timu hiyo, alitimiza ahadi hiyo juzi katika hafla fupi ya kukabidhi mfano wa cheki iliyofanyika juzi usiku, Dar es Salaam.


"Wachezaji 16 walipewa sh. milioni moja kila mmoja, na maofisa sita wa timu walipewa sh. 800,000 kila mmoja, hivyo kufanya jumla ya sh. milioni 20.8," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Akizungumza na wachezaji hao, viongozi wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), na baadhi ya Wake wa Viongozi ambao ni wanachama wa New Millenium Women Group, Mama Pinda aliwapongeza wachezaji hao kwa jinsi walivyojituma na kufanikiwa kushika nafasi ya pili.

Aliwataka wachezaji hao kuzidi kujituma zaidi hata katika mashindano yatakayofanyika mwakani nchini Malawi na kwamba walifanya kazi kubwa kuifunga timu ngumu kama Botswana.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wachezaji wenzake, nahodha wa timu hiyo, Lilian Sylidion alisema ahadi ya Mama Pinda ambayo aliitoa wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo iliwapa hamasa na kuchochea kupatikana kwa ushindi huo.





No comments:

Post a Comment