15 May 2012

Kim awarudisha Bocco, Samatta Taifa Stars *Nsajigwa, Henry, Nizar waachwa



Na Zahoro Mlanzi

KOCHA mpya wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen amemrudisha kikosi mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco 'Adebayor' ambaye alitangaza kustaafu kuchezea timu hiyo pamoja na Mbwana Samatta wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya kuwa nje ya kikosi kwa muda.

Mbali na hilo, aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa kwa mara ya kwanza ameachwa katika kikosi hicho kutokana na kushuka kwa kiwango huku wachezaji wa nje, Henry Joseph, Athuman Machupa, Ali Badru Ali na Nizar Khalfan nao wakiachwa.

Lakini katika kikosi cha hicho ambacho kina wachezaji 25, wameitwa kwa mara ya kwanza wachezaji vijana wa timu ya Simba, Edward Christopher, Jonas Jerald na Ramadhan Singano pamoja na Frank Domayo wa JKT Ruvu na Simon Msuva wa Moro United.

Akitangaza kikosi hicho Dar es Salaam jana, Kim alisema anashukuru kwanza kuona Benchi la Ufundi limebaki kama lilivyo kwani watu waliopo anawajua vizuri na amefanya nao kazi, hivyo hakutakuwa na tatizo.

"Silyvester Marsh (kocha msaidizi) na Pondamali (kocha wa makipa) ninawajua vizuri na kikubwa katika kikosi changu nimeita wachezaji kutokana na uwezo, ufundi, uwajibikaji, nidhamu pamoja na uwiano wa wachezaji," alisema Kim na kuongeza;

"Najua watu watakuwa na maswali kwani nimewajumuisha wachezaji wengi vijana U-20, nimefanya hivyo kutokana na uwezo na vipaji walivyonavyo hivyo kama hawatatusaidia leo najua watatusaidia kwa baadaye na si kujali umri wao".

Aliwataja wachezaji hao ni makipa, Juman Kaseja, Mwadin Ali na Deogratius Munishi, mabeki ni Said Nassor, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Juma Nyosso, Wazir Salum na Amir Maftah.

Viungo ni Mwinyi Kazimoto, Abubakari Salum, Nurdin Bakari, Shaaban Nditi na Mrisho Ngassa na washambuliaji ni Thomas Ulimwengu na Haruna Moshi 'Boban'.

Akizungumzia kuhusu suala la Bocco, Kim alisema ameshazungumza naye na amekubali kuchezea Taifa Stars huku lile la wachezaji wa nje kuita wachache alisema kwa sasa hawaitaji ila atakapowaitaji atawaita.

Pia kuhusu Nsajigwa na beki Nadir Haroub 'Canavaro', alisema wamekuwa na kipindi kibaya katika kumalizia ligi hivyo wana nafasi endapo wataonesha mabadiliko katika uchezaji wao.

Kikosi hicho kinatarajiwa kuanza mazoezi Jumatano asubuhi kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Malawi na ile ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2014 ambapo Juni 2, mwaka huu itacheza na Ivory Coast.

No comments:

Post a Comment