15 May 2012
Wazee Yanga watamba wana milioni 750/- kibindoni *Ally Mayai naye abwaga manyanga
Na Elizabeth Mayemba
SIKU moja baada ya Vijana wa Yanga kumuangukia aliyekuwa Mfadhili wa timu hiyo, Yusuph Manji, Wazee wa Baraza la Muafaka wa klabu hiyo, wameamua kuweka hadharani akaunti yao kuwa ina sh. milioni 750 kwa ajili ya kumaliza matatizo yanayoikabili timu yao.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa baraza hilo, Ibrahim Akilimali alisema fedha hizo ni kwa ajili ya kulipa madeni ya wachezaji, watumishi wote, usajili pamoja na timu kuiweka kambini kwa ajili ya michuano ya kombe la Kagame.
Alisema hawataki kuonana na Mwenyekiti wa timu hiyo, Llody Nchunga katika tarehe aliyopanga ambayo ni Mei 20, mwaka huu kwakuwa hawana chakuzungumza naye.
"Kama ni mkutano basi utakuwa wa wanachama wote siku hiyo ambayo Nchunga amepanga na pia utakuwa wa kumuondoa na wapo tayari kugharamia kila kitu siku hiyo," alisema Mzee Akilimali.
Alisema yote watafanya hayo endapo Nchunga atajiweka pembeni na pia wamewazuia wanachama kulipa ada ya uanachama mpaka atakapoondoka mwenyekiti huyo.
Pia wamemtaka aliyekuwa mfadhili wao Yusuph Manji kutotoa kiasi cha sh.milioni 12 alizokuwa akitoa kila mwisho wa mwezi na mwezi uliopita ndio uwe mwisho wake kutoa fedha hizo.
Akilimali alisema pia wanamuomba Ridhiwani Kikwete ambaye wanadai alimleta Nchunga awasaidie kumuondoa mwenyekiti huyo kwa maslahi ya timu.
Klabu hiyo hivi sasa ipo katika mvutano mkubwa kati ya uongozi uliopo chini ya Nchunga na Wazee na Vijana wa klabu hiyo ambapo wanashinikiza Nchunga ajiuzulu kutokana na kudai kushindwa kuiongoza timu.
Wazee na Vijana hao wanadai kwamba amesababisha timu kuwa na madeni makubwa huku wakiwa na wasiwasi huenda asifanye usajili mzuri hususani katika michuano ya Kombe la Kagame, hivyo wanataka ang'atuke.
Wakati huo huo inadaiwa kuwa, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Ally Mayai naye amejiuzulu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment