24 May 2012

Kichocho bado tishio hapa nchini-Dkt.Njau


Na Mwandishi Wetu, Mwanza

WATU milioni 200 duniani wameambukizwa ugonjwa wa kichocho cha kibofu na tumbo katika nchi 76 huku wengine milioni 700 wakiwa katika hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa huo.

Utafiti unaonesha kwamba kati ya watu 10 waliopimwa sita walibainika kuambukizwa ugonjwa wa kichocho cha tumbo hapa nchini ambapo kulingana na viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO) maambukizi hayo ni ya kiwango cha hali ya juu hivyo hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.


Ugonjwa wa kichocho kwa upande wa hapa nchini unaonesha kuwaathiri zaidi wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ambako magonjwa aina zote mbili yanapatikana katika maeneo ya mikoa hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Kituo cha Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) mkoani Mwanza Dkt. Mansweat Njau wakati akifungua mkutano wa kwanza kwa wadau wa mradi wa utafiti wa ugonjwa wa kichocho cha tumbo jijini Mwanza.

Alisema ugonjwa wa kichocho umeenea sana hapa nchini hasa katika Kanda ya Ziwa Victoria ambao huwathiri sana watoto wa umri wa kwenda shule, wasichana na akinamama wenye umri wa kujifungua, watu wazima na wavuvi.

Alisema, ugonjwa wa kichocho hasa kichocho cha tumbo una madhara makubwa kiafya kwa watoto na watu wazima walioambukizwa na huchangia kupunguza uwezo wa watoto kujifunza na kuongeza umaskini katika jamii.

“Kituo chetu kinatekeleza mradi mkubwa wa SCORE, kufanya utafiti wa ugonjwa wa kichocho cha tumbo kwa watoto wa umri wa kwenda shule pamoja na jamii katika vijiji 150 vya Mkoa wa Mwanza, vilivyopo kando kando ya Ziwa Victoria. Njia sahihi ya kudhibiti ugonjwa huu na kupunguza madhara yanayotokana na mambukizi ni kutibu kwa kutumia dawa aina ya prziquantel,”alisema Dkt. Njau.

Alisema, mradi huo wa SCORE utatekelezwa katika wilaya sita za mkoa wa Mwanza ambapo vijiji 150 vitanufaika katika wilaya za Magu ( 37), Misungwi (4), Nyamagana (7), Ilemela (9), Sengerema (55)na Geita (38).

Alieleza kuwa tangu kuanza kwa mradi huo ambao utakamilika mwaka 2015 kwa kupima na kutoa tiba katika vijiji hivyo 150 hadi sasa jumla ya watoto wa shule wapatao 27,926 na watu wazima 5,446 wamepimwa na kutokana na upimaji huo wastani wa maambukizi ya ugonjwa wa kichocho cha tumbo yalikuwa ni asilimia 60 hadi 100 kiwango ambacho ni kikubwa.

Dkt. Njau alisema lengo la SCORE ni kufanya utafiti ili kuboresha mkakatii wa kupambana na ugonjwa wa kichocho cha tumbo ikiwa ni pamoja na kutoa matibabu.

Mradi huo umelenga pia kutoa mchango mkubwa katika jitihada za kupambana na ugonjwa wa kichocho Tanzania na dunaini kote.

Kwa mujibu wa Dkt. Njau mradi wa SCORE utahudumia mikoa sita ya Geita Mwanza, Mara, Shinyanga, Simiyu na Kagera ili kupata takwimu za Kanda kwa ajili ya utafiti kwa kutumia wataalamu wake ambao watashirikiana na vituo vingine vya utafiti duniani.

No comments:

Post a Comment