17 May 2012

Bomoabomoa fukweni iende sambamba na udhibiti hati bandia



JUZI Serikali kupitia Wizara  ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ilitangaza  imetangaza kwamba nyumba zote zilizojengwa kandokando ya fukwe za bahari na mito zitabomolewa bila wamiliki kulipwa fidia kutokana na kukiuka Sheria za Ardhi na Mazingira za mwaka 1992, 1995 na 2004.

Taarifa hiyo ilitolewa kwa pamoja na mawaziri i katika Wizara hiyo, Prof. Anna Tibaijuka na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa, walipozungumza na waandishi wa habari kuelezea migogoro ya ardhi inayotokea nchini na mikakati ya wizara zao kutatua migogoro hiyo.

Prof. Tibaijuka, alisema zoezi la kuwahamisha wakazi waliojenga kandokando ya fukwe za bahari litahusisha mikoa yote iliyopakana na Bahari ya Hindi ambayo ni Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara kwa kuzingatia sheria zilizowekwa ambazo zinakataza ujenzi wa nyumba kandokando ya fukwe za bahari ndani ya mita 60 pamoja na mita 30 kandokando ya mto.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa, alisema kuwa zoezi la kuwahamisha wakazi waliovamia mito linatarajiwa kuanza hivi karibuni na wataanza na wakazi waliovamia mto Mbezi na Nduwe.

Alisema Setelaiti ya mwaka 2005 inaonyesha mto Ndumbwi ulikuwa unaonekana wazi, lakini sasa wakazi wameuvamia na kujenga kandokando ya mto huo, hata Mto Mbezi Beach pia

Alisema kuwa ukaguzi kwa wakazi waliojenga ndani ya mita 30 kutoka kandokando ya mito utafanyika hivi karibuni sambamba na zoezi la kuwabomolea nyumba zao.

Tunaunga mkono tamko hilo la mawaziri hao kwani ni lazima tufuate sheria zinazokataza kujenga kandokando ya fukwe za bahari, kwani hizo ni sehemu maalum kwa watu wote kuzitumia

Hii ni kutokana na kwamba kwa  kujenga kandokando ya fukwe za bahari na mito ni hatari kwa maisha kutokana na kuwa tumeshuhudia athari zilizotokea pindi tsunami ilipoikumba nchi yetu, pamoja na mafuriko

Hatua hiyo ya wizara ni njema kutokana na kwamba ina lengo la kuzuia majanga yanayoweza kulikabili taifa endapo yatatokea majanga kama ya tsunami na  kupasuka kingo za mito pindi yanapotokea mafuriko.


Hata hivyo pamoja na nia njema ya wizara tunachukua fursa hii kuiomba oparesheni hiyo iende sambamba na udhibiti wa utoaji hati  za kumiliki viwanja kiolela kwani  ndicho chanzo cha kuibuka ujenzi huo.

Tumeshuhudia majengo mengi yakiota kama uyoga katika maeneo mbalimbali ya nchi hususani fukweni mwa bahari na mito,huku wahusika wakiyafumbia macho .

Tuna imani kama wizara itadhibiti uchakachuaji wa hati za viwanja kwa kiasi kikubwa itasaidia kukomesha tatizo hilo.



No comments:

Post a Comment