15 May 2012

Asasi yaaswa kuzingatia uwazi na uwajibikaji


Na Godwin Msalichuma

VIONGOZI wa Asasi Isiyokuwa ya Kiserikali ya MYAAG wilayani Mtwara mkoani Mtwara wameaswa kuzingatia matumizi mazuri ya ruzuku walizopata kutekeleza mradi wa kinga dhidi ya VVU pamoja na watu wanye ulemavu ili ziwafikie walengwa hao.


Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na Ofisa Tarafa ya Ziwani wilayani
humo Bw. Francis Mkuti alipokuwa akizindua rasmi mradi huo ambao
utahusisha watu wenye ulemavu na ulifanyika mjini hapa.

Bw. Mkuti alisema kupata ruzuku kutoka kwa mfuko wa ukimwi wa Rapid
Funding Envelop ni jambo moja na matumizi ya uwazi kwa walengwa
na wadau ni jambo jingine.

“Unapokosa uwazi kwa walengwa wa mradi juu ya matumizi ya pesa
unakaribisha minong’ono ambayo mwishowe ni kusambaratika kwa watendaji
na magomvi baina ya viongozi wa asasi…kusiwe na mficho katika matumizi
ya fedha za mradi hapo mtaepuka migogoro na pia mtawavutia wafadhili
kuweza kufanya kazi na nyinyi hapo mbele,” alisema Bw. Mkuti.

Mratibu wa mradi huo Bw. Kassim Chikwenga alisema mradi ni wa mwaka
mmoja ambapo wamepata ufadhili kutoka mfuko wa ukimwi mzunguko wa tisa
unaoitwa Rapid Funding Envelop (RFE) ambapo ni wa kinga ya virusi vya
ukimwi miongoni mwa walemavu ambao wanategemea kuwafikia walengwa
1,250.

“MYAAG ni asasi ya vijana inayojishughulisha na masuala ya afya na
kuwahudumia waoto wanaoishi katika mazingira hatarishi zaidi, lakini
pia inajishughulisha na watu waishio na virusi vya Ukimwi, lengo letu
kuu ni kupambana na maambukizi mapya pamoja na unyanyapaa ambao
umekuwa kikwazo cha wengine kujitangaza,” alisema Bw. Chikwenga.

Naye meneja wa mradi huo Bw. Winnie Mwakalaba alisema kuwa
wanachokiomba kwa jamii ni ushirikiano katika kuweza kutekeleza kwa
kipindi chote cha mradi huo kwani mara nyingi jamii imekuwa ikisema
kuwa ni wa asasi wakati mrardi uliandaliwa kwa kuishirikisha jamii hiyo
jambo ambalo huachiwa shirika lililoandaa matokeo yake makusudi
hayafikiwi.

No comments:

Post a Comment